Tumbatu FM

Masheha zibeni njia zinazoeneza matendo maovu

14 June 2024, 12:30 pm

Picha ya Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Siti Abasi Ali akiwa katika kikao cha pamoja na masheha wa wilaya ya kati.

Kudhibiti maeneo hatarishi kutapunguza kuenea kwa matukio ya udhalilishaji wa kijinsia.

Na Vuai Juma.

Masheha wa Wilaya ya Kati wametakiwa kuwatafuta wamiliki wa maboma na nyumba za kukodisha katika Shehia  zao ili kuziba mianya ya  vitendo viovu katika jamii .

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Siti Abasi Ali ametoa wito huo Dunga Wilaya ya Kati wakati alipokuwa akizungumza na masheha hao pamoja na kujadili mbinu mbalimbali zitakazoweza kuondosha matendo hayo.

Amesema kuwa yapo majengo ambayo yamekuwa yakitumika  kufanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye maeneo hayo ambavyo vinasababisha athari katika jamii.

Aidha amewataka kufanya kazi kwa pamoja na  Waratibu wa jinsia katika shehia zao   ili kuweze kukomeshwa kwa kadhia hiyo inayowakumba wanawake na watoto.

Kwa uapande wake Katibu wa Masheha wa Wilaya ya Kati Zidi Suleiman amesema watahakikisha wanaendelea kutoa  ushirikiano wa kutosha kwa Waratibu hao licha ya  kazi ngumu wanayoifanya usiku na mchana.