Tumbatu FM
Tumbatu FM
4 September 2025, 6:11 pm

“Ikiwa watu wenye ulemavu watawekewa mazingi rafiki ya kufika kwenye vituo vya kupigia kura kuwezesha kutokuwepo kwa mtu yoyote mwenye ulemavu kukosa fursa ya kupiga kura”
Na Juma Haji.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kaskazini Unguja Bi Mboja Hesabu ameishauri Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuzingatia mazingira ya watu wenye ulemavu katika matayarisho ya shughuli za Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Akifungua kongomano la wadu wa maendeleo jumuishi katika jamii kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mattar Zahor Masoud lililofanyika Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini A, amesema watu wenye ulemavu wanahitaji mazingira maalum tofauti na makundi mengine ya jamii ambapo hulazimu kuongozwa ili kufika kwenye vituo vya kupigia kura.
Akifafanua zaidi, amesema ZEC inapaswa kuzingatia uteuzi bora wa vituo vya kupigia kura pamoja na kuweka wakalimani wa lugha ya alama kwenye vituo hivyo ili kusaidia watu wenye ulemavu kupiga kura kwa urahisi.
Awali wakiwasilisha salamu za Shirikisho la Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Zanzibar Shijuwaza mwenyekiti wa shirikisho hilo Ali Omar Makame amesema watu wenye ulemavu wanakabiliwa na hofu ya kutojua mifumo mipya ya uchaguzi na kuiomba tume ya uchaguzi kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara ili kuondokana na wasiwasi wa kufanya maamuzi ya kuwapigia kura wagombea wasiokuwa chaguo lao.
Akifunga kongomano hilo Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Kaskazini A Abdulmajid Ramadhan Zamiri, amewataka waandishi wa habari za uchaguzi kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja kuwashirikisha watu wenye ulemavu kwenye vipindi vya mijadala ya elimu ya mpiga kura ili kupata uzoefu wa kujenga hoja katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Kongomano la wadau wa maendeleo jumuishi la mwaka 2025 limeandaliwa na Shirikisho la Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) kwa kushirikiana na baraza la taifa la watu wenye ulemavu kwa ufadhili wa The Norwegian Asociation of Disabled (NAD).