Ruangwa FM

DC Ngoma apongeza kiwango cha mafunzo yanayotolewa na jeshi la akiba Ruangwa

27 August 2025, 11:12 pm

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, amepongeza kiwango cha mafunzo yaliyotolewa kwa Askari wa Jeshi la Akiba katika Kata ya Mandawa, akisema yamekuwa ya mfano na chachu ya kuimarisha ulinzi na mshikamano wa wananchi.

Mhe. Ngoma ametoa kauli hiyo leo, Agosti 26, 2025, wakati akihitimisha sherehe za kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mchichili, ambapo jumla ya vijana 109 wamehitimu, wakiwemo wanaume 91 na wanawake 18.

Katika hotuba yake, Mkuu huyo wa Wilaya amewapongeza vijana hao kwa nidhamu na uvumilivu waliouonesha katika kipindi cha mafunzo, akiwataka kuendelea kuwa walinzi wa amani na kushirikiana na Serikali katika kulinda usalama wa jamii.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa Ruangwa na Tanzania kwa ujumla kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 kwa amani na utulivu, akisisitiza kuwa mshikamano na ushiriki wa kila mmoja ni msingi wa demokrasia imara.

Kwa upande wake, Meja H.A. Mwakaninyamale, Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Ruangwa, amesema mafunzo hayo yaliyodumu kwa majuma 18 yamehusisha mbinu za ulinzi wa Taifa, utayari wa kijeshi, pamoja na mafunzo ya uokoaji kwa vitendo na nadharia.

Wananchi waliohudhuria sherehe hizo wameeleza kufurahishwa na kiwango cha mafunzo pamoja na mshirikiano wa Jeshi la Akiba na jamii, wakisema hatua hiyo inaimarisha imani ya usalama na mshikamano wa kijamii.