Ruangwa FM

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atangaza rasmi kutogombea tena Ubunge Ruangwa

2 July 2025, 8:39 pm

Na Loveness Joseph.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, leo Julai 2, 2025, ametangaza rasmi kutogombea tena nafasi ya ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu ujao, baada ya kulitumikia kwa kipindi cha miaka 15.

Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Lindi na Wilaya ya Ruangwa, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Ruangwa kwa kumuunga mkono na kushirikiana naye katika kipindi chote cha uongozi wake tangu mwaka 2010.

“Umefika wakati kwa mshikamano tulioujenga sasa ni wakati wa kutoa fursa kwa Wanaruangwa wengine wapenda maendeleo waweze kuunganisha nguvu hizi ili kaulimbiu yetu ya Ruangwa kwa Maendeleo Inawezekana iweze kusonga mbele zaidi,” amesema Majaliwa

Aidha, ametoa wito kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya kuwapa ushirikiano wagombea wote watakaojitokeza kuwania ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akisistiza umuhimu wa kudumisha mshikamano na utulivu wakati wa mchakato wa kisiasa.

Sauti ya waziri mkuu Kassimu Majaliwa.

Katika salamu zake kwa wananchi, Mheshimiwa Majaliwa amewasihi Wanaruangwa kuendelea kushikamana na kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni, kusikiliza sera za wagombea, na hatimaye kuwachagua kwa kura za kutosha wagombea wa CCM, akiwemo Mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Vilevile, ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wakuu wa CCM kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kulitumikia jimbo la Ruangwa kwa muda mrefu.

Aidha kwa upande wa wilaya ya ruangwa wamejitokeza wagombea watano kuwania nafasi ya ubunge jimboni hapo ambao tayari wamekwisha rudisha fomu ikiwa ni Mparuka Hashimu Mtopela Mkulima na Mjasiriamali,Philip Undile Makotha ambae ni Engeneer,Wakili Fikiri Bonface Liganga,Bakari Nampenya Kalembo ambae ni mjumbe wa bodi Ngorongoro pamoja na Kaspar Kaspar Mmuya DAS.