Ruangwa FM
Ruangwa FM
12 June 2025, 3:16 pm

Katika Maonesho ya Pili ya Madini ya Mkoa wa Lindi (Lindi Mining Expo 2025), Meneja wa TANESCO Mkoa wa Lindi, Bw.Theodory Hall amewataka wananchi kuachana na matumizi ya mkaa na kuni na badala yake kutumia vifaa vya umeme vya kisasa vya kupikia kama vile pressure cooker, rice cooker, na jagi la umeme.

“Kwa kutumia kifaa cha kisasa, mwananchi anaweza kupika kwa kutumia unit moja ya umeme kwa siku nzima – ni nafuu zaidi kuliko kutumia mkaa,” alisema Bw. Hall.
TANESCO inashiriki kikamilifu katika maonesho hayo kuelimisha jamii juu ya nishati safi na mbadala wa gharama nafuu kwa matumizi ya majumbani.
Aidha, alibainisha kuwa Wizara ya Nishati imetoa kibali kwa wasambazaji wazawakueneza vifaa hivyo nchini kote.
Kwa mujibu wa TANESCO, iwapo kifaa kitapata hitilafu, mteja anaweza kukirudisha kwa ajili ya matengenezo au kubadilishiwa.
Mpango huu ni sehemu ya mkakati wa kitaifa unaolenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, kila Mtanzania anatumia nishati safi, salama na nafuu kwa ajili ya kupikia.
ikiwa leo 12Jun 2025 ni siku ya pili ya maonesho ya madini na fursa za uwekezaji mkoa wa lindi yenye kauli mbiu isemayo “Madini na Uwekezaji Fursa ya Kiuchumi Lindi.Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025”.