Ruangwa FM

Mama Samia Legal Aid yafikia wananchi zaidi ya millioni1

19 February 2025, 8:14 pm

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza ruangwa

Na Loveness Daniel

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni ubunifu wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan uliolenga kuongeza wigo wa upatikanaji haki kwa wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za huduma za kisheria.

Amesema kuwa kupitia kampeni hiyo ambayo inatolewa bure mpaka sasa imefanikiwa kuwafikia zaidi ya wananchi milioni moja wakiwemo wanawake 681,326 na wanaume 691,773 katika mikoa 19 nchini.

Amesema hayo leo Jumatano (Februari 19, 2025) wakati alipozindua kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika mkoa wa Lindi, kwenye viwanja vya Madini, Ruangwa Mkoani Lindi.

Ameongeza kuwa kupitia kampeni hii migogoro mbalimbali ya ardhi, ndoa, mirathi imetatuliwa. “Ni ukweli isiopingika kuwa, jamii nyingi zimekuwa na changamoto kuhusu mirathi ambazo zinachangia kuondoa amani miongoni mwa wanandugu kwa kugombania mali.”

Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuwa kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia unasifa nne ambazo ni umuhimu wake kwa jamii, umaalum wake ni kwasababu inatelekeza maelekezo ya Rais Dkt. Samia, umahususi wake imeasisiwa na Rais Dkt. Samia “ukipekee wake ni kwasabau inatekeleza falsafa ya R4”

Kwa Upande wake Naibu Waziri Katiba na Sheria Jumanne Sagini amesema kuwa Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wananchi wanaifikia haki kwa wakati na kwa ufanisi.

Amesema kuwa ili kuhakikisha lengo hilo linawezekana, Wizara imeendela kutoa mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria na kujenga uwezo kwa watoa huduma za msaada wa kisheria ili kuendelea kusogeza zaidi huduma hizo karibu na wananchi.

“Mwezi Desemba, 2024, Wizara iliingia makubaliano na Chama cha Wanasheria Tanganyika kwa lengo la kuimarisha zaidi huduma za uwakili kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili”