Mwalimu afungwa jela maisha kubaka mtoto wa miaka 7
5 September 2024, 6:04 pm
Na Khadja Omary
Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Lindi imemuhukumu Hassan Saddi, mwenye umri wa miaka (28) mkazi wa Mchinga Mkoani Lindi kutumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela na kumlipa muhanga fidia ya shilingi Laki Tano (500,000/=) kwa kosa la kumbaka Mtoto wa miaka Saba (7) Mwanafunzi wa Darasa la Kwanza.
Hukumu hiyo ya kesi namba 15710 ya mwaka 2024 imetolewa Septemba 03, 2024 na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Mhe. Delphina Kimath huku upande wa Mashtaka ukiongozwa na John Remy na Hadija Mwambungu.
Inaelezwa Mtuhumiwa alikuwa ni mwalimu wa kujitolea kwenye shule ya Msingi Mchinga na kwamba alitenda kosa hilo Mei 19, 2024 majira ya Saa Kumi na Moja na dakika Ishirini Jioni huko katika kijiji cha Mchinga wilaya ya Lindi baada ya kumrubuni kwa kumuonyesha picha za ngono Mtoto huyo wakiwa nae nyumbani kwake kisha kutekeleza tukio hilo la kumbaka.