Ruangwa FM

Nimefurahishwa na miradi ya kimaendeleo – Majaliwa

22 February 2023, 7:40 pm

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema anafurahishwa na mafanikio makubwa ya utekelezwaji wa ujenzi miradi mbalimbali ya maendeleo yanayoonekana katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

“Wana-Ruangwa lazima tuendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha nyingi za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Haya ni mafanikio makubwa, Ruangwa kwa maendeleo inawezekana.”

Amesema hayo leo (Jumatano, Februari 22, 2022) baada ya kukagua ujenzi wa jengo la utawala shule ya Sekondari ya Wasichana Ruangwa (Ruangwa Girls) pamoja na madarasa katika Shule ya Sekondari ya Kitandi wilayani Ruangwa.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anaridhia kutoa fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu mbalimbali ya utoaji huduma za jamii hapa nchini hivyo ni jukumu la kila wananchi ni kuitunza ili ilete faida anayoikusudia

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wanafunzi kwamba wajitahidi kufanya vizuri kwenye masomo yao “Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameweka mkazo katika elimu, ambayo inatolewa bure kuanzia awali hadi kidato cha sita”

Naye Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Telak amewataka wazazi wawape watoto nafasi ya kushiriki kikamilifu katika masomo ili waweze kutimiza ndoto zao

 “Jitahidini kufanya vizuri kitaaluma, mjitambue nyie ni wanafunzi na hivyo mjiepushe na vishawishi vyovyote vitakavyokwamisha maendeleo yenu kitaaluma. Wananchi tuwalinde watoto wetu ili watimize ndoto zao. Mtoto wa mwenzio ni wako.”

Pia, Waziri Mkuu amewataka wananchi kuacha kuvamia maeneo ya karibu kwa kuwa Serikali imeyahifadhi kwa ajili matumizi ya baadae ya taasisi husika. “Hapa palikuwa pori hapakuwa na shamba pasiguswe.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekagua ujenzi wa madarasa ya ghorofa yanayojengwa katika shule ya msingi Likangara, ambapo ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa ubunifu wa mradi huo. Mradi huo unahusisha vyumba vinane vya madarasa, matundu 24 ya vyoo na ofisini nne.