

March 4, 2025, 6:36 pm
“Ninawasihi sana uongozi wa shule hii, walimu na wote mnaohusika kutokengeuka na kugeuza matumizi ya gari hili ambalo nimelikabidhi leo kwa kuanza kuikodisha au kuifanya kuwa daladala badala yake ikafanye kazi kulingana na malengo yaliyokusudiwa”
Na Sebastian Mnakaya
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha ameutaka uongozi wa shule ya sekondari ya Mwl. Nyerere katika Halmashauri ya Msalala kutogeuza matumizi ya gari la kubebea wagonjwa (school ambulance) kuwa daladala, kuikodisha au kuifanya ya biashara kwa namna yoyote ile kwani kufanya hivyo ni kinyume na lengo lililokusudiwa.
Macha ameyasema haya katika hafla ya kukabidhi gari hilo ambapo pamoja na yote amewapongeza Wazazi, Bodi ya Shule pamoja na Wadau wa Elimu kwa kushiriki katika uchangiaji wa ununuzi wa gari hilo lililogharimu zaidi ya Tzs. Milioni 26.
Aidha Macha ameutaka uongozi wa shule hiyo kuweka utaratibu mzuri wa namna la kulihudumia na kulitunza, huku akimwagiza mkuu wa jeshi la polisi Msalala kulifanyia ukaguzi kabla ya kuanza kutumia.
Nae Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mwalimu Nyerere Mwl. Kafuru Songora ameahidi kulitunza na kulisimamia gari hilo ili litumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili lidumu kwa muda mrefu na kuwasaidia wanafunzi wanaokumbwa na changamoto za kiafya hususani kidato cha tano na sita ambao wanakaa bwenini.
Mbunge wa Jimbo la Msalala Idd Kassim ameahidi kutoa tofali 1000 kwa ajili ya kujenga Chumba Maalum cha watoto wa kike na Mashine ya kuvuta maji (motor) ambayo itakayokuwa ikitumika kuvuta maji katika kisima kinachotarajiwa kujengwa shuleni hapo, huku mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Msalala Rose Manumba amesema wataendelea kukamilisha miundombinu ya shule hiyo kadri fedha zitakavyopatika.
Shule ya sekondari Mwalimu Nyerere ina jumla ya wanafunzi 1,523 na wavulana wakiwa 520 na wasichana 1003 wanafunzi hao ni wakutwa na bweni ambao wanaanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.