Kahama FM
Kahama FM
March 17, 2026, 1:30 pm

”Huduma ya niashati ya umeme kwa mtaa wa Lugel-Mtakuja unatarajiwa kufika katika eneo hilo hivi karibuni”
Na Sebastian Mnakaya
Wananchi wa mtaa wa Mtakuja kata ya Nyahanga wilayani Kahama mkoani Shinynga, wanatarajia kupatiwa huduma ya nishati ya umeme katika maeneo ambayo bado huduma hiyo haijafika.
Akizungumza katika kikao na wananchi wa Lugela –Mtakuja, wakati wakipatiwa elimu ya namna ya kuunganishiwa umeme katika makazi yao na maafisa kutoka TANESCO, diwani wa kata ya Nyahanga Josephine Kilimba, amesema hatua ya kwanza ni kupatiwa elimu ili umeme unapofika kila mtu awe na sifa za kuunganishwa umeme.

Aidha, Kilimba ameliomba shirika hilo kuwasaidia wananchi kupata umeme kwa haraka bila ya kuwa na namba za viwanja ili wakazi hao wafikiwe na huduma hiyo bila ya kuwa na masharti magumu wa upatikanaji wa nishati hiyo.

Mkuu wa kitengo cha huduma kwa wateja uhusiano na mahusiano kwa umma TANESCO wilaya Kahama Robart Msemo, amewataka wananchi hao kujiandaa kupatiwa huduma hiyo ya umeme kwa kufanya maandalizi ya kuweka mifumo ya umeme kwenye nyumba zao.

Nae, mwenyekiti wa mtaa wa Mtakuja Mohamed Lumala ameishukuru serikali kwa jitihada za kuwapatia huduma ya umeme kwa mtaa huo ikiwa ni changamoto ya muda mrefu, huku mkazi wa mtaa huo Dora Marwa akiomba utekelezaji wa mradi huo uwafikie kwa wakati katika maeneo hayo.