Kahama FM

Zaidi ya mita za maji 542 zaibwa Kahama

July 23, 2025, 2:20 pm

Mita za maji mpya baada ya zile za zamani kuibwa (Picha na Sebastian Mnakaya)

Matukio ya wizi wa mita za maji katika mji wa Kahama yameshamiri katika kata ya Nyahanga, Malunga, Majengo na Mhongolo, hali inayosababisha wananchi kukosa maji

Na Sebastian Mnakaya

Zaidi ya mita za maji 542 zimeripotiwa kuibwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, huku wananchi wakitakiwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kukomesha wizi huo.

Wito huo umetolewa leo na Afisa Mahusiano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) John Mkama wakati akizungumza na Kahama FM, ambapo amesema matukio hayo ya wizi wa mita za maji yameshamiri katika kata za Nyahanga, Malunga, Majengo na Mhongolo, hali inayosababisha wananchi kukosa maji.

Sauti ya Afisa mahusiano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) John Mkama
Afisa mahusiano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) John Mkama

Aidha, Mkama amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa KUWASA ili kuwakamata wanaoiba mita hizo, huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi amesema mpaka sasa wamewakamata watu kadhaa kuhusiana na matukio hayo na bado upelelezi unaendelea.

Sauti ya Afisa mahusiano wa KUWASA John Mkama na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga (SACP) Janeth Magomi

Kwa upande wao baadhi ya wananchi walioibiwa mita hizo za maji akiwemo Prica Vicent na Mtaa wa Nyahanga na Paulo Kisuzi wa Mtaa wa Igomelo, wakizungumza kwa nyakati tofauti wameomba serikali kukomesha tabia hiyo ya wizi wa mita za maji, ambapo wananchi wanapata hasara kwa kununua mita mpya.

Sauti ya Prica Vicent Mtaa wa Nyahanga na Paulo Kisuzi wa mtaa wa Igomelo
Prica Vicent na mkazi Mtaa wa Nyahanga Manispaa ya Kahama

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Kahama akiwemo Jumanne Kasuku na Samweli Binda wamehoji juu ya mita hizo zinazoibwa zinapelekwa wapi na kwa kazi gani, huku wakiiomba serkali kutatua chamamoto hiyo, ambayo kila siku wizi huo unaendelea katika maeneo mbalimbali ya mji wa Kahama.

Sauti ya Jumanne Kasuku na Samweli Binda wakazi wa Manispaa ya Kahama
Mzee Jumanne Kasuku mkazi wa Nyahanga
Samweli Binda mkazi wa Kata ya Nyahanga