Kahama FM

Uzalishaji wa zao la pamba umeendelea kuimarika nchini

May 6, 2025, 1:58 pm

Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa (Picha na Sebastian Mnakaya)

”Zao la pamba umeendelea kuimarika nchini, ambapo hadi sasa umeongezeka kutoka tani 180,000 hadi kufikia tani 400,000”

Na Sebastian Mnakaya

Serikali imesema uzalishaji wa zao la pamba umeendelea kuimarika nchini, ambapo hadi sasa umeongezeka kutoka tani 180,000 hadi kufikia tani 400,000, ikiwa ni hatua kubwa kuelekea lengo la kufikia uzalishaji wa tani milioni moja ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Shinyanga, Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya kilimo zimeanza kuzaa matunda.

Msigwa amesema Serikali imejipanga kuhakikisha inafanikisha lengo hilo kwa kuboresha huduma kwa wakulima, ikiwemo kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Sauti ya Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wakulima, wataalamu wa kilimo na wadau wengine kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa ya kisasa na yenye mchango mkubwa kwa uchumi wa Taifa.