

March 16, 2025, 9:54 pm
Vijiji na kata zote zinazopita mradi wa bomba la maji kutoka ziwa vitoria, mkandarasi atakiwa kuwapatia kazi wananchi ili kujikwamua kiuchumi pamoja na kunufaika na mradi huo
Na sebastian Mnakaya
Mkandarasi wa Kampuni ya Sihotech Engineering Ltd anayetekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa Victoria unaojengwa kuanzia Manispaa ya Kahama kwenda Halmashauri ya Ushetu (km 68.2) ametakiwa kutoa baadhi ya kazi kwa wazawa kwenye maeneo ya mradi unapopita ili kuwanufaisha kwa kuongeza vipato vyao.
Agizo hilo limetolewa leo na mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita wakati kifanya ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya mradi huo, ambapo amemtaka mkandarasi huyo kutoa kazi kwa utaratibu katika eneo la mradi unapopita kupata fursa kwa wananchi kushiriki.
Aidha, Mhita amesema kuwa kabla ya kazi ya kuchimba mitaro na kusambaza mabomba kuanza wanapaswa kuwashirikisha wananchi wa maeneo ya mradi ili nao waweze kunufaika, huku mradi huo utakao dumu kwa mwezi 24 kukamilika kwake.
Nae, kaimu meneja wa RUWASA wilaya ya Kahama Mhandisi Mkama amesema mkandasi ameendelea na utaratibu wa kutoa fursa za kazi kwa wazawa, huku Meneja mradi wa Sihotech Engineering Mhandisi Hagai Mziray amesema wameendelea kutekeleza maagizo ya serikali ya kutoa fursa za kazi kwa wananchi na kuwataka kuendelea kijitokeza.
Baadhi ya wananchi wa halmashauri ya Ushetu wakizungumza kwa nyakati tofauti, akiwemo Nicolas Maganga amesema kukamilika kwa mradi huo utawasaidi kutokutembea mbali mrefu wa kutafuta maji pamoja na kupata fursa za ajira, huku Elizabeth Simon amesema itawasaidia kutekeleza shughuli za nyumbani kwa wakati kutokana na maji kuwa karibu.
Ujenzi wa Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 44, na kwa awamu ya kwanza utavifikia vijiji 54 kwenye kata 11 kati ya kata 20 zilizopo katika halmashauri Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga.