Kahama FM

Wanawake wachimbaji walia na rushwa ya ngono migodini Kahama

July 22, 2024, 6:30 pm

Mmoja wa wanawake wanaojishughulisha na uchimbaji mdogo wa madini

Wanawake kutokuwa na mitaji mikubwa kunafanya waingie katika vishawishi vya rushwa ya ngono ili kukidhi mitaji yao.

Na William Bundala Kahama

Wanawake wanaojishughulisha na uchimbaji mdogo wa madini wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamesema kuwa wanakumbuna na changamoto nyingi katika shughuli za uchimbaji ikiwemo kuwa na mitaji midogo hali inayowafanya waombwe rushwa ya ngono ili kukidhi mahitaji katika sekta ya uchimbaji wa madini.

Wamebainisha hayo leo kwa nyakati tofauti katika machimbo madogo ya dhahabu wilayani Kahama kuhusu changamoto wanazokutana nazo wanawake wanaofanya shughuli za uchimbaji mdogo katika wilaya ya Kahama.

Sauti za wanawake

Wanawake hao wamesema kuwa kutokuwa na mitaji mikubwa kunafanya waingie katika vishawishi vya rushwa ya ngono ili kukidhi mitaji yao huku wakiiomba serikali kuruhusu mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa elimu migodini pamoja na kuandaa sera na sheria zitakazowasaidia wanawake katika sekta ya uchimbaji wa madini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mgodi wa Ntambalale namba 4 uliopo halmashauri ya Msalala Zacharia Soko amesema kuwa ili wanawake wanaojishughulisha na uchimbaji mdogo waondokane na rushwa ya ngono serikali iwape kipaumbele kwenye mikopo ili wapate mitaji na kuwatengenezea vikundi na kutoa wito kwa wamiliki wa leseni za uchimbaji kote nchini kuwapa nafasi wanawake katika sekta ya uchimbaji bila kuangalia jinsia zao.

Awali akizungumza na Kahama FM, afisa mawasiliano wa shirika lisilo la kiserikali la Hakirasilimali linaloshughulika na mafuta,M madini na gesi Shakira Zaidi amesema kuwa shirika lao limeamua kuja na  mradi unaolenga kuibua changamoto ambazo  wanapitia wanawake katika uchimbaji mdogo wa madini ili kuwasaidia wanawake na kutatua changamoto zao ikiwa ni pamoja  na kuwatengenezea sera na sheria za kuwaongoza katika sehemu zao za uchimbaji.