Kahama FM

Naibu Waziri Kapinga awahakikishia umeme wananchi wa vijiji vya Manzwagi, Kidunyashi

July 4, 2024, 4:39 pm

Naibu Waziri wa Nishati. Mhe. Judith Kapinga akizungumza katika ziara yake kwenye Vijiji vya Manzwagi na Kidunyashi 

Naibu Waziri wa Nishati. Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea kuwasimamia kwa umakini wakandarasi ili waweze kukamilisha kazi zao kwa wakati na kwa ufanisi, pia amewaelekeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha wanaongeza nguzo 40 ambazo ni Sawa na kilometa mbili kwa wananchi wa vijiji vya Manzwagi na Kidunyashi kabla ya tarehe 27 Julai, 2024.

Mhe. Kapinga amesema hayo tarehe 03 Julai, 2024 alipokuwa anahitimisha ziara yake katika Wilaya ya Kahama kwenye Vijiji vya Manzwagi na Kidunyashi vilivyopo Wilaya ya Kahama Mjini Mkoani Shinyanga.

Kapinga amesema Vijiji hivyo vitafikiwa na Nishati ya Umeme mwezi huu wa julai 2024 ambapo kijiji cha Manzwagi kitapata umeme ifikapo tarehe 14 julai na kijiji cha Kidunyashi kitapatiwa umeme ifikapo tarehe 10 julai, 2024.

Amesema kutokana na suala la maendeleo kuwa ni hatua, Serikali iliweka nguvu kubwa katika usambazaji wa umeme vijijini na sasa hatua inayofuata ni kupeleka umeme vitongojini ili kuwezesha shughuli za kijamii na kiuchumi.

Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Julius Mtatiro  ameshukuru kazi kubwa ya usambazaji umeme inayofanywa katika maeneo mbalimbali na pia amempongeza Mbunge wa Kahama Mjini Mhe. Jumanne Kishimba kwa kuwajali Wananchi kwa kuwapatia Maendeleo kwa wakati.