Fedha za ununuzi wa pamba ni mkopo kutoka TADB
June 11, 2024, 7:00 pm
Chama kikuu cha KACU kimepokea mkopo wa shilingi bilioni tisa na milioni miatano kwa ajili ya kununua pamba kwa msimu wa 2024/2025 ambapo kinatarajia kununua pamba kilo milioni 6.
Na Leokadia Andrew
Chama kikuu cha ushirika KACU wilayani Kahama mkoani Shinyanga kimewataka viongozi wa vyama vya msingi vya pamba kuwa waaminifu na kusimamia vizuri ununuzi wa pamba kwa msimu wa masoko 2024/2025.
Wito huo umetolewa leo na mwenyekiti wa chama kikuu cha KACU Emmanuel Nyambi wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya msingi vya pamba na tumbaku.
Nyambi amesema kuwa fedha za ununuzi wa pamba ni mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na kuwataka viongozi kufuata taratibu na miongozo iliyotolewa ya matumizi sahihi ya fedha hizo.
Kwa upande wake Mkaguzi wa pamba wilaya ya Kahama Emmanuel Kileo amewataka viongozi kuacha kuwakata wakulima madeni ya mikopo ya pembejeo kwakuwa serikali imesamehe madeni ya pembejeo kwa wakulima pamba.
Nao baadhi ya Viongozi wa vyama vya msingi vya Pamba wamehaidi kutekeleza yote walioagizwa na Chama kikuu cha Ushirika (KACU) na wametoa shukrani kwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan kufuta madeni ya Pembejeo kwakuwa msimu uliopita mvua ziliharibu mazao yao.
Chama kikuu cha KACU kimepokea mkopo wa shilingi bilioni tisa na milioni miatano kwa ajili ya kununua pamba kwa msimu wa 2024/2025 ambapo kinatarajia kununua pamba kilo milioni 6.