ushetu
Kahama FM

KAHAMA:Cherehani atoa Fedha za Mifuko 58 ya Saruji,kata ya Sabasabini Ushetu.

December 7, 2021, 4:32 pm

Wananchi wa Kitongoji cha Imalange kata ya Sabasabini Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wamemshukuru mbunge wa Jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi Milioni moja na laki tatu kwa ajili ya kununua mifuko 58 ya saruji  ya ujenzi wa boma la vyumba vya madarasa mawili katika shule ya Msingi Imalange.

Wakiongea kwa nyakati tofauti na Kahama Fm wananchi hao wamesema kuwa kwa muda mrefu watoto wao wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwenda shuleni katika shule shikizi ya Imalange na kwamba ujenzi wa Shule hiyo mpya utasaidia watoto wao kwenda umbali mfupi kupata elimu.

Sambamba na hayo wamesema kuwa shule Shikizi ya Imalange inakabiliwa na changamto nyingi ikiwemo uwepo wa wanyama wakali kama fisi hali inayohatarisha uhai wa wanafunzi pindi wanapotoka au kwenda shuleni.

Kwa upande wake Mbunge wa Ushetu Emmanuel Cherehani amewasisitiza Viongozi wa Kijiji na wadau wa elimu wa kata ya Sabasabini kusimamia fedha hizo kwa uadilifu ili zikafanye kazi iliyokusudiwa na kutoa wito kwa wazazi kuwahimiza watoto wao kupenda shule kwani Elimu ndiyo urithi pekee wa mtoto.

Mbunge wa Ushetu Emmanuel Cherehani akiongea na Viongozi na wananchi wa Kitongoji cha Imalange Kata ya Sabasabini.

Cherehani ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejidhatiti kikamilifu katika kuboresha Elimu Tanzania hivyo viongozi na wananchi ni vyema wakamuunga mkono ili kutoa elimu bora kwa wanafunzi wote nchini.

Shule Shikizi ya Imalange inawanafunzi wa darasa moja la awali ambalo lina wanafunzi zaidi ya 200 hali inayopelekea wanafunzi wengine kusomea nje ya darasa.

Cherehani ametoa fedha hizo katika ziara  yake ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo lake la Ushetu.

Msingi wa vyumba viwili vya Madarasa Shule ya Msingi Imalange ambao Cherehani ametoa Mifuko 58 ya Saruji ili kuanza ujenzi wa Maboma.