NUKTA AFRICA:Waandishi wa wa habari za mitandaoni andikeni habari zenye tija.
November 1, 2021, 2:07 pm
DAR ES SALAAM
Waandishi wa habari za mitandao wametakiwa kuandika habari zenye ubora ikiwa ni pamoja na kutumia takwimu za uhakika ili kutoa taarifa sahihi kwa wasomaji na kuacha tabia ya kuangalia idadi ya wasomaji na watu waliotembelea mitandao yao.
Wito huo umetolewa leo jiji Dar es salaam na Mkurugenzi mtendaji wa Nukta Africa Nuzulack Dausen katika mafunzo ya uhakiki wa habari yaliyoandaliwa na Tanzania Media Foundation (TMF).
Dausen amesema kuwa kwasasa waandishi wengi wa Mitandaoni wanaandika habari zisizo na vigezo vya habari huku wakiacha maswala mengi ya muhimu zikiwemo Takwimu,mizani na ukweli.
Ameongeza kuwa wamiliki wengi wa vyombo vya habari mitandaoni wanajali kuangalia idadi ya watu waliotembelea mitandao yao bila kuangalia kama habari walizoweka zimesaidia kuleta mafanikio chanya katika jamii.
Sambamba na hao Dausen amesema kuwa kwasasa wasomaji wa mitandao wameanza kuzikwepa taarifa zenye vichwa vya habari vya kuvutia ambavyo haviendani na uhalisia wa habari zenyewe.
Awali akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi mtendaji wa Tanzania Media Foundation (TMF) Dastan Kamanzi amesema kuwa waandishi wa habari wanatakiwa kuwa na Msingi wa awali,Msingi wa Jumla na msingi wa kubobea katika uandikaji wa habari katika jamii.
Kamanzi amesema kuwa msingi wa uandishi wa habari ni ukweli hivyo ni muhimu waandishi wa habari kuzingatia msingi huo kila wanapoaandika habari zao.
Mafunzo hayo ya ufatiliaji wa habari yamejumuisha waandishi wa habari za mitandaoni Kutoka Mikoa ya Shinyanga,Tabora,Mwanza,Arusha,Dodoma,Mbeya,Mara na Iringa.