KAHAMA:Makamu wa Rais wa CODEPATA atembelea ofisi ya Maendeleo ya jamii.
October 12, 2021, 11:01 am
Makamu wa Rais wa Chama Cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA) Dr. Regina Malima ametembelea ofisi za Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kahama wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
Katika ziara yake amefanikiwa kufanya kikao na Mratibu wa Kanda ya Ziwa Ndugu DISMAS LWOMILE pamoja na watumishi wa Idara hiyo.
Agenda kubwa ya ziara hiyo ilikuwa ni kufahamiana na pia kujadiliana masuala mbalimbali ya Chama ikiwemo kuhamasisha wanachama wapya na kutambua Taasisi mbalimbali zenye wafanyakazi ambao ni Wataalam wa kada ya Maendeleo ya Jamii Kanda ya Ziwa.
Mratibu Dismas Lwebugisa amekiri kuwa na idadi ya wanachama wapatao 120 kwa Kanda ya Ziwa na kubainisha mikakati mbalimbali waliyonayo kwa Kanda ya Ziwa ikiwemo kuongeza wanachama wapya.
Agenda nyingine ilikuwa ni kuhamasishana ktk kujipanga na kujiandaa kwa mkutano mkuu wa Chama utakaofanyika mapema February 2022.
Katika kuhitimisha kikao hicho Dr Malima amewashukuru Wataalam hao kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Manispaa ya Kahama na kuifanya wilaya hiyo kuwa ya mfano nchini katika masuala la Uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Makam huyo wa Rais kwa niaba ya viongozi wenzake ameahidi kushirikiana nao kwa karibu na kupanga kikao kingine hivi karibuni ili kujadili kwa kina masuala mbalimbali ya Chama na namna bora ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ametoa rai kwa wanachama wote nchini kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na viongozi wa Chama ili kuleta tija na mafanikio makubwa ya kitaaluma na maendeleo ya jamii ya watanzania.
Kwa upande wao wafanyakazi wa Idara ya ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kahama wamemshukuru Makamu wa Rais wa CODEPATA Dr. Regina Malima kwa kuwatembelea na kuahidi kuwa mstari wa mbele katika kukipigania Chama kwa kuwa na mikakati endekevu ikiwemo kutafuta wanachama wapya.
Chama cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA) kilianza mwaka 2017 na kupata usajili Namba S.A 21457 na Kwa Sasa kina wanachama zaidi ya 400 nchini Tanzania huku Kanda ya ziwa kikiwa na jumla ya wanachama 120,Chama hiki Cha kitaaluma kiko chini ya ulezi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.