Wafanyabiashara Kahama waziomba mamlaka za afya kuendelea kutoa elimu ya kujikinga na UVIKO 19.
August 18, 2021, 9:15 pm
Baadhi ya wafanyabiashara katika soko la Namanga lililopo Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga wameiomba serikali kuendelea kutoa elimu ya kujikinga na UVIKO 19 kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
Wakizungumza na KAHAMA FM wafanyabiashara hao wamesema licha ya elimu kutolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari, baadhi yao bado hawaamini uvaaji wa barakoa katika kujinga na UVIKO 19.
Aidha wafanyabiashara wamesema katika soko la Namanga wana utaratibu wa kunawa mikono kwa maji tiririka na uvaaji barakoa wakati wa kuingia pamoja na kutumia vipukusi (sanitizer).
Kwa upande wake mwenyekiti wa afya LUCAS KIBELA amesema wameweka maji tiririka pamoja na sabuni maeneo ya kuingia ndani ya soko, huku zoezi la usafi hufanyika mara mbili kwa mwezi.
Ikumbukwe kwamba chanjo Inaendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali ikiwemo hosiptali ya Manspaa Kahama,kituo cha afya Mwendakulima,zahanati ya Kagongwa na kituo cha afya Iyenze.