Kahama FM

OSHA YAZINDUA MPANGO WA KUSAJILI NA KUKAGUA MAENEO YA WAJASIRIAMALI WADOGO.

May 31, 2021, 1:48 pm

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umezindua mpango maalum wa kuwasajili na kuwahudumia wajasiriamali wadogo kupitia ukaguzi wa sehemu za kazi, kuwapa mafunzo na ushauri wa kitaalam kuhusiana na masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.

Mpango huo umezinduliwa rasmi katika maonesho ya wajasiriamali na wawekezaji yaliyohitimishwa mwishoni mwa wiki katika kituo cha uwezeshaji wananchi kiuchumi mjini Kahama mkoani Shinyanga.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema mpango huo mahsusi umeandaliwa na Taasisi yake baada ya kuendesha programu ya mafunzo kwa wajasiriamali wadogo kwa miaka mitano na kubainisha ombwe katika usimamizi wa usalama na afya miongoni mwa kundi hilo muhimu. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa GS1 Tanzania ambao ndio waratibu wa maonesho hayo kwa kushirikiana na kituo cha uwezeshaji wananchi kiuchumi Kahama, Fatma Kange, amesema Taasisi yake inashirikiana na OSHA katika kuwawezesha wajasiriamali kukuza biashara zao pamoja na kuwapa miongozo ya kuboresha mazingira yao ya kazi.

Baadhi ya wajasiriamali walioshiriki katika maonesho hayo na kupata fursa ya kusajili maeneo yao ya kazi pamoja na kupatiwa mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi wameeleza jinsi walivyoupokea mpango huo pamoja na mafunzo waliyoyapata.

OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambayo husimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Majukumu yake ya msingi ni pamoja na kusajili maeneo ya kazi, kufanya kaguzi za usalama na afya mahali pa kazi, kuchunguza afya za wafanyakazi, kufanya tafiti na kuishauri serikali kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.