Madiwani Kishapu waazimia kumsimamisha kazi mweka hazina.
April 23, 2021, 7:54 am
WIKI Kadhaa baada ya ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuipa hati ya mashaka Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Madiwani wa halmashauri hiyo kwa kauli moja wameazimia kumsimamisha kazi Mweka hazina wa halmashauri hiyo, Deus Ngelanizya kwa kosa la kushindwa kusimamia mapato ya mwaka wa fedhan 2020/2021 na kusababishia halmashauri hiyo kuwa ya mwisho kitaifa kwenye makusanyo ya nusu mwaka.
Madiwani hao wamesema kuwa mweka hazina huyo anapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kusimamishwa kazi kwa makosa ya kuzarau maagizo ya madiwani na kuisababishia halmashauri kupata hati ya mashaka kwa mwaka 2019 /2020, huku afisa mipango wa halmashauri hiyo Mang’era Mang’era akitakiwa kujitathimini utendaji kazi wake wa kazi kwa sababu anajukumu la kufuatilia mipango yote ya halmashauri hiyo.
Maazimio hayo yamefikiwa jana Aprili 21, 2021 kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo baada ya baraza hilo kukaa kama kamati na kujadili juu ya wafanyakazi hao.
Akitangaza maazimio ya madiwani hao, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, William Jijimya ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mondo, amesema wameamua kutoa maazimio hayo kwa sababu wameshindwa kusimamia kikamilifu mapato ya halmashauri hiyo, hali ambayo wameisababishia kupata hati ya mashaka na kuwa ya mwisho kitaifa.
Naye Diwani wa Kata ya Mwamalasa, Bushi Mpina alisema wameamua kuwaadhimia watumishi hao kwa sababu hawasimamii fedha kikamilifu, fedha zinaingia lakini hawajui inaenda wapi hivyo wameona ukusanyaji unaofanywa sio sahihi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Emmanuel Jonhson amesema kama inatokea changamoto ya kusababisha hati ya mashaka idara ya fedha ilitakiwa kusaidiwa, kutoa ushauri na kuwa weledi katika suala la mapato, pia unahitajika ushirikiano wa hali ya juu katika kusimamia mapato.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kengese amesema ni jambo la aibu kuona halmashauri hiyo ina kuwa ya mwisho kitaifa na kupata hati ya mashaka, hivyo watumishi wote wanatakiwa kujituma katika kusimamia mapato na kuongeza vyanzo mbadala kwa ajili ya kuongeza mapato.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga, Lucas Nyanda amewapongeza kwa kusimamia vizuri maendeleo ya wananchi kwa sababu sifa ya kiongozi ni kuonyesha njia, lakini katika kusomeka kwa kupata hati ya mashaka haikutakiwa kufikia hatua hiyo, ni vizuri kutengeneza mazingira mazuri ili mapato yaweze kuongezeka.