Mwanafunzi wa darasa la kwanza aliwa na mamba Ziwa Victoria.
April 6, 2021, 7:49 am
Janeti Mganga (8) aliyekuwa anasoma darasa la kwanza shule ya msingi Busikimbili iliyoko kata ya Maisome, Halmashauri ya Buchosa, wilayani Sengerema mkoani Mwanza ameuawa na mamba wakati akioga kwenye Ziwa Victoria huku baadhi ya viungo vya mwili wake vikiwa vimenyofolewa na kutafunwa na mamba huyo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole, amesema mwanafunzi huyo alikutwa na tukio hilo wakati alipokua akioga na wanafunzi wenzake katika Ziwa Victoria.
Kipole amewasihi wazazi wasiwaruhusu watoto wao kwenda kuogelea ziwani badala yake wateke maji na kwenda majumbani.
Diwani wa Kata ya Maisome, Dauson Miyaga amechukizwa na visa vya mamba kuendelea kugharimu maisha ya watu na kuzitaka mamlaka husika kuchukuwa hatua juu ya mamba hao.
Wakati Ofisa mtendaji Kijiji cha Busikimbi, Salimu Magayi amesema wamesikitishwa na kifo hicho na kueleza huenda mwanafunzi huyo pengine angekuwa kiongozi katika siku za usoni.
Amewaomba wananchi wawe wavumilivu kwani wao wapo kwa ajili ya kusaidia wananchi ikiwemo kutatua kero zilizopo katika jamii.
Wakati Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Busikimbi, Kosmas Makoye alithibitisha tukio la mwanafunzi kuliwa na mamba.
Wiribeti Mangapera, ambaye ni mkazi wa Kata ya Maisome ameeleza kuwa visa vya mamba kula watu vimekuwa vikiongezeka kila siku na hivi karibuni walimpoteza Raulensia Igayo, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kisaba ambacho ni kijiji jirani na Busikimbi.