Unyanja FM

Selikali kupambana na imani potofu dhidi ya wenye ulemavu

1 October 2026, 1:18 pm

Picha ni mwana saikolojia kutoka hospitali ya wilaya ya Nyasa

Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau mbalimbali katika kutoa elimu kuhusu ualbino, bado watu wenye ualbino wanaendelea kukabiliwa na changamoto ya unyanyapaa, ubaguzi na mitazamo hasi kutoka kwa baadhi ya wanajamii.

Na Godlove Matiku

Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau mbalimbali katika kutoa elimu kuhusu ualbino, bado watu wenye ualbino wanaendelea kukabiliwa na changamoto ya unyanyapaa, ubaguzi na mitazamo hasi kutoka kwa baadhi ya wanajamii.

Baadhi ya wananchi Mkoa wa Ruvuma  bado wanaamini kuwa watu wenye ualbino wana nguvu za kimiujiza, ni ishara ya bahati au mkosi, au kwamba viungo vyao vinaweza kutumika katika imani za kishirikina ili kupata utajiri.

Imani hizo potofu zinaendelea kuchochea hofu, ubaguzi na kuwafanya baadhi ya watu wenye ualbino kuishi kwa tahadhari, huku wakikosa uhuru wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii.

Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ualbino Wilaya ya Nyasa, Ezekiel Matembo , amesema ingawa matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino yamepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali, bado kuna changamoto ya mila na imani potofu zinazoendelea kuwepo katika baadhi ya maeneo.

Amesema hali hiyo inaendelea kuwanyima baadhi ya watu wenye ualbino haki ya kuishi kwa usawa, usalama na kuheshimiwa kama wananchi wengine.

Sauti ya mwenyekiti chama cha ualbino

Kwa upande wake, Mwanasaikolojia Chrispin Zumbwe kutoka Hospitali ya Wilaya, amesema lugha za kejeli, unyanyapaa na ubaguzi vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya akili ya watu wenye ualbino.

Amesema madhara hayo yanaweza kujumuisha msongo wa mawazo, kupungua kwa kujiamini, hofu ya kushiriki katika shughuli za kijamii na wakati mwingine huzuni ya muda mrefu, hasa kwa watoto na vijana wanaokulia katika mazingira ya kunyanyapaliwa.

Sauti ya mwanasaikolojia

Baadhi ya wananchi wamesema bado kuna watu wanaoshikilia imani hizo potofu kutokana na mila na desturi zilizopitwa na wakati, pamoja na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu ualbino.

Wamesema ni muhimu elimu zaidi kutolewa katika jamii ili kuondoa dhana potofu kuhusu watu wenye ualbino na kuwajengea mazingira salama ya kuishi na kushiriki katika shughuli mbalimbali bila hofu au ubaguzi.

Sauti za wananchi

Wadau wa haki za binadamu wamehimiza viongozi wa dini, viongozi wa kimila, wazazi, walimu na vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu sahihi kuhusu ualbino na kukemea imani potofu zinazochochea ubaguzi na unyanyapaa.

Wamesisitiza umuhimu wa kuhakikisha watu wenye ualbino wanalindwa, wanaheshimiwa na wanapata fursa sawa katika elimu, ajira, huduma za afya na shughuli za maendeleo ya jamii bila ubaguzi.