Tumbatu FM

Kuelekea uchaguzi mkuu, TADIO yaipiga msasa Tumbatu FM

11 December 2024, 7:54 am

Wafanyakazi wa radio jamii Tumbatu FM pamoja na Mhariri wa Radio Tadio Hilali Ruhundwa (aliyevaa miwani) wakiwa katika mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la Habari za Maendeleo Tanzania (TADIO).

Picha na Sheha Haji.

Ikiwa waandishi wa habari wataandika habari zinazohusu masuala ya uchaguzi kwa kuzingatia taaluma yao ya uandishi wa habari wataweza kuepusha jamii na uvunjifu wa amani”

Na Sheha Haji

Watendaji wa Redio Jamii Tumbatu FM wametakiwa kuzingatia maadili wakati wa kuripoti habari za uchaguzi ili kuiepusha jamii kuingia kwenye migogoro isiyo ya lazima.

Akitoa mafunzo ya siku moja kwa wafanyakazi wa Redio hiyo huko Wilaya Ndogo Tumbatu, mhariri kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Radio za Jamii Tanzania (TADIO) Bw. Hilali Ruhundwa amesema utoaji wa taarifa zisizo sahihi katika kipindi cha uchaguzi unaweza kusababisha kuvunjika kwa amani iliyopo nchini, hivyo amewataka waandishi kutafuta vyanzo vya uhakika ili kupata taarifa sahihi kwa manufaaya jamii.

Akizungumzia majukumu ya redio za kijamii nchini, amesema ni muhimu kwa redio hizo kuripoti habari za ndani ya jamii husika ili kuwanufaisha walengwa.

Hata hivyo amefahamisha kuwa, dunia inakabiliwa na mabadiliko makubwa ya teknolojia ya habari hivyo amezitaka redio jamii nchini kuyatumia vyema majukwaa ya mitandaoni katika utoaji wa taarifa ili kuwafikia watu wengi zaidi.

Nao viongozi na waandishi wa Redio Jamii Tumbatu FM wameishukuru TADIO Kwa kuwapatia mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa maendeleo ya redio hiyo.

Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Vyombo vya Habari wa Finland (VIKES) chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo kupitia TADIO.

TADIO inaundwa na redio za jamii zaidi ya 42 nchini Tanzania na imekuwa ikitoa mafunzo kwa redio wanachama kuendana na kasi ya teknolojia ya sasa.