Tumbatu FM

Wananchi fuateni misingi ya dini

5 July 2024, 4:58 pm

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika kongamano la wanawake wa kiislam. Picha na Vuai Juma.

Iwapo wananchi wataweka mbele imani ya dini kutapelekea kuondosha uvunjifu wa amani.

Na Vuai Juma.

Wananchi wa Tanzania wametakiwa kufuata misingi ya dini ili  kuepusha mifarakano ambayo itapelekea uvunjifu wa amani iliyopo.

Wito huo umetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Kongamano la Wanawake wa Kiislamu kufuatia maadhimisho ya mwaka mpya wa kiislam 1446 al-Hijra lililoandaliwa na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar katika hoteli ya  Golden Tulip Uwanja wa Ndege  .

Amesema iwapo jamii itafuata misingi ya dini kutapelekea kumuweka mtu katika heshma, uadilifu na Imani ya ucha Mungu itakayompelekea kumuogopa Mwenyezi Mungu kwa kuwa mwema na kuepukana na mifarakano.

Hata Hivyo Amesema wapo baadhi ya watu wanaokiuka misingi ya dini zao na kutamka maneno mabaya na matusi kwa viongozi jambo ambalo halikubaliki kwani huchochea kuleta mifarakano ndani ya nchini.

Adha ameitaka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kusimamia waganga wajadi ili kuweza kuachana na ramli chonganyishi  kwani kufanya hivyo kutasababisha maafa kwa jamii .

Na Vuai Juma.

Picha ya katibu mtendaji wa ofisi ya mufti mkuu wa Zanzibar Sheikh Halid Ali Mfaume akihutubia kwenye kongamano la wanawake wa kiislam.

Mapema Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume amesema Kongamano la Mwaka Mpya wa Kiislamu limeanzia Pemba kwa shughuli mbali mbali Tarehe 26/6/ 2024 na linatarajiwa kufungwa  kesho na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussen Ali Mwinyi  katika Msikiti wa Jamii Zinjibar Mazizini Zanzibar.