

March 4, 2025, 4:37 pm
Siku moja baada ya kuripotiwa kifo cha mwanamke mwenye ualbino Wande Mbiti mkazi wa kijiji cha Nhelegani kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga ambaye mwili wake umekutwa ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi huku mlango ukiwa umefungwa kwa nje, Mkuu wa Wilaya hiyo Wakili Julius Mtatiro amewataka wananchi kutoa ushirikiano ili uchunguzi wa tukio hilo uweze kufanikiwa.
Na Sebstian Mnakaya
Wananchi katika Manispaa ya Shinyanga wamewatakiwa kutoa ushirikiano katika kifo cha mwanamke mwenye ualbino Wande Mbiti mkazi wa kijiji cha Nhelegani ili uchunguzi wa tukio hilo ufanikiwe.
Kauli hiyo inakuja ikiwa ni siku moja baada ya kuripotiwa kifo cha mwanamke huyo ambaye mwili wake umekutwa ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi huku mlango ukiwa umefungwa kwa nje.
Mkuu wa Wilaya hiyo Wakili Julius Mtatiro amesema hayo wakati akitoa pole, ambapo amesema uchunguzi wa awali wa daktari umeonesha marehemu hana viashiria vyovyote vinavyoonesha kushambuliwa na hivyo uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini mazingira ya tukio hilo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kizumbi Reuben Kitinya amesema moja ya kitu walichokibaini baada ya kuvunja kufuli na kuingia ndani ni nguo za marehemu kutokuwepo na kwamba alikutwa kitandani akiwa bila nguo huku baba mzazi wa marehemu Mbiti Kulwa akiliomba jeshi la polisi kufanya upelelezi haraka ili kubaini chanzo cha binti yake kupoteza maisha.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Kennedy Mgani, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa tayari uchunguzi wa awali umefanyika, na kwamba upelelezi unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho.
Tukio hilo limebainika Machi 02 mwaka huu, baada ya majirani kuhisi harufu kali, huku mlango ukiwa umefungwa na kufuli kwa nje ndipo walipotoa taarifa kwa uongozi wa kijiji, ambao nao ulilazimika kuvunja dirisha ndipo walipomuona mwanamke huyo akiwa amelala kitandani.