Kahama FM

Halmashauri ya Ushetu yazindua rasmi Chanjo ya Polio

March 26, 2026, 12:03 pm

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu, Hadija Kabojela azindua zoezi la chanjo ya polio

”Chanjo ya Polio ni salama, imehakikiwa kitaalamu, na hutolewa bila malipo yoyote, hivyo hakuna sababu kwa mzazi au mlezi kushindwa kumpeleka mtoto wake kupata huduma hiyo muhimu”

Sebastian Mnakaya

Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga imezindua rasmi kampeni ya chanjo ya Polio yenye lengo la kuwalinda watoto dhidi ya ugonjwa huo hatari, ambapo zaidi ya watoto 148,000 wenye umri chini ya miaka 10 wanatarajiwa kufikiwa katika zoezi hilo.

Uzinduzi huo umefanyika katika Shule ya Msingi Nyamilangano, ukiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Hadija Kabojela, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kabojela amesema kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hususan ugonjwa wa Polio ambao unaathiri afya na ustawi wa watoto.

Aidha, amesisitiza kuwa ni muhimu kwa jamii kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha watoto wote wanaostahili wanapatiwa chanjo hiyo kwa wakati.

Sauti ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Hadija Kabojela

Amefafanua kuwa chanjo ya Polio ni salama, imehakikiwa kitaalamu, na hutolewa bila malipo yoyote, hivyo hakuna sababu kwa mzazi au mlezi kushindwa kumpeleka mtoto wake kupata huduma hiyo muhimu.

Zoezi la utoaji chanjo litaendelea katika kata zote ndani ya Halmashauri ya Ushetu, ambapo timu za wataalamu wa afya zitawafikia watoto katika maeneo mbalimbali ikiwemo vituo vya afya, zahanati pamoja na maeneo ya mikusanyiko ya jamii.