Kahama FM
Kahama FM
February 14, 2026, 10:26 am

”Kata ya Nyahanga ina shule za msingi tano, huku ikiwa na shule moja ya sekondari ambayo imekuwa ikipokea wanafunzi wengi hali inayosababisa kuongeza shule nyingine ya pili ili kuondokana na changamoto kuwa na wanafunzi wengi”
Diwani wa kata ya Nyahanga, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga Josephina Kilimba ameiomba serikali kujenga shule ya sekondari ya pili katika kata hiyo ili kupunguza idadi kubwa kwa wanafunzi.
Kilimba ameyasema hayo leo, katika kikao cha baraza la madiwani Manispaa ya Kahama wakati wa kuchangia na kujadili rasimu ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ambapo amesema kata ya Nyahanga ina shule ya sekondari moja, ambayo imekuwa na wanafunzi wengi na kuiomba serikali kujenga shule nyingine ili kupunguza wingi wa wanafunzi hao.

Aidha, Kilimba amesema katika sekta elimu, kuna changamoto ya matundu ya vyoo kwa shule ya msingi Luluma katika kata ya Busoko na shule ya Nyahanga B, huku katika shule ya Kinaga na Nduku ikiwa na uhaba wa walimu, madawati na kuomba serikali kutenga fedha katika bajeti hiyo ili kutatua changamoto hizo.

Nae, mkuu wa idara ya Mipango Manispaa ya Kahama Flora Sangiwa, akijibu swali la diwani wa Nyahanga amesema serikali kwa sasa umeanza mpango wa kujenga mabweni katika shule ya sekondari Seeke ili kupunguza msongamano huo, huku serikali ikiweka mpango wa kujenga shule ya sekondari mwaka wa fedha ujao.
Leo baraza la madiwa la Manispaa ya Kahama limepitisha rasimu ya makisio ya Mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027 shilingi billion 70, ambapo bajeti hiyo inatarajiwa kukusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali, ikiwemo mapato ya ndani, ruzuku kutoka serikali kuu pamoj na michango ya wananchi.