Jeshi la polisi Shinyanga lawakamata watuhumiwa mauaji
June 11, 2024, 6:48 pm
“Hatutakubali matendo haya ya kikatili yaendelee ndani ya Mkoa wa Shinyanga kwahiyo jeshi la Polisi tumeingia katika oparesheni kali kabisa kuhakikisha kwamba tunawasaka wale wote ambao wamehusika katika matendo haya na kwa kuanzia sasahivi tunawatuhumiwa watatu mparoni kuhusiana na lile tukio la mwanzo ambalo lilitokea katika kijiji cha Iwelyangula na Bugayambelele kata za Kitangili na Kizumbi na hawa watuhumiwa ni wakazi wa Mkoa wa Shinyanga sisi tutawapeleleza mpaka pale ambalo tutahakikisha jarada lao tunalifikisha kwa wanasheria halafu tuweze kupisha makahama”.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewakamata watuhumiwa watatu wanaohusishwa na mauji ya watu wawili waliouawa na kisha kuchomwa moto kwa tuhuma za wizi katika kata za Kitangili na Kizumbi Manispaa ya Shinyanga.
Taarifa hiyo imetolewa na kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi wakati akizungumza na Misalaba Media, ambapo amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni mafanikio yanayotokana na msako na doria mbalimbali zinazofanywa na askari wa jeshi hilo.
Amesema jeshi hilo halitawafumbia macho wale wote wanaobainika kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watuhumiwa wa matukio ya uhalifu kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi.
Kamanda Magomi amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi kutoa taarifa za matukio ya wahalifu na uhalifu badala ya kujichukulia sheria mkononi.