Wananchi halmashauri ya Ushetu kunufaika na hifadhi ya Kigosi
July 10, 2023, 11:35 pm
Serikali imegawa hifadhi ya Kigosi iliyopo katika halmashauri ya Ushetu takriban kilometa 7,000 kwa ajili ya wananchi kufanya shughuli mbalimbali
Na Sebastian Mnakaya
Wananchi wa halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga watanufaika na hifadhi ya Kigosi baada ya serikali kumega kilometa 7,000 ya eneo hilo kuwa chini ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ambapo wananchi wataruhusiwa kufanya shughuli za kimaendeleo.
Akizungumza katika sherehe za kumpomgeza Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Hassan katika kata ya Ulowa mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa Livingstone Lusinde amesema jambo hilo limekuwa likizungumzwa mara kwa mara na mbunge wa jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani juu ya changamato la pori hilo hali iliyosababisha kubadilishiwa matumizi.
Kwa upande wake, mbunge wa jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani, amesema kabla ya serikali kumega eneo hilo kwa wananchi walikuwa hawaruhusiwi kufanya shughuli zozote za kimaendeleo, ambapo kwa sasa wataendelea na shughuli hizo bila ya kuwa na vikwazo vyovyote.
Naye, makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Ushetu Doa Limbo ameishukuru serikali kwa kutatua mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka kumi, ambapo kwa sasa wananchi watanufaika na eneo hilo kwa shughuli za kimaendeleo.
Aidha diwani wa kata ya Ulowa Gabrela Kimaro amesema kuwa kwa kurudishwa pori hilo chini ya usimamizi wa TFS itasaidia wananchi wengi kujipatia kipato kwa kufanya shughuli za ufugaji na uvuvi.
Awali pori hilo lilikuwa chini ya Wakala wa Misitu Tanzania {TFS}, na mwaka 2019 likapandishwa hadhi kuwa chini ya usimamizi wa Hifadhi za Taifa Tanzania [TANAPA] ambapo hifadhi hiyo ilikuwa inazuia shughuli za kiuchumi kufanyika ndani ya pori hilo hali iliyosababisha mgogoro na wananchi wa eneo hilo.