Kahama FM

KAHAMA: halmashauri ya Msalala kupokea zaidi ya shilingi bilioni mbili.

November 4, 2021, 4:06 pm

Serikali imetoa  fedha kiasi cha shilingi bilioni mbili na milioni  mia nne na kumi,kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, ikiwa ni fedha za ustawi wa maendeleo ya Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19.

Afisa  mipango  wa halmashauri hiyo  ELIKANA ZABRON  amesema hayo katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani kilichofanyika leo,katika ukumbi wa halmashauri ya Msalala.

ZABRON amesema fedha hizo ambazo zimetolewa na serikali ya awamu ya sita chini ya rais SAMIA SULUHU HASSAN katika kutekeleza adhima ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo zitaenda kutekeleza sekta ya elimu msingi na sekondari pamoja na afya.

Aidha kupitia wizara ya afya, halmashauri hiyo itapokea  magari mawili, ambapo gari la kwanza ni kwa ajili ya kubeba wagonjwa (ambulance) na gari la pili ni kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji shughuli za afya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri hiyo FRANSIS FUSSI amewataka madiwani kwenda kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia fedha hizo  za mapambano dhidi ya UVIKO 19.