Kahama FM

Kahama:Mwanamke aliyejulikana kwa jina la LIMI KULWA (30) ameuawa kwa kukatwa na panga.

September 28, 2021, 11:14 am

kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando

Mwanamke aliyejulikana kwa jina la LIMI KULWA (30) mkazi wa kijiji cha Ilunga kata ya Iyenze wilayani Kahama amefariki dunia baada ya kukatwa na panga sehemu mbalimbali za mwili wake na mume wake, huku Chanzo cha mauaji hayo kikitajwa kuwa ni imani za kishirikina.

Taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP GEORGE KYANDO imeeleza kuwa tukio hilo limetokea jana Septemba 27 2021 majira ya saa 2:30 usiku katika kijiji hicho cha Ilunga kata ya Iyenze wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

KYANDO ameeleza kuwa mtuhumiwa huyo ambaye ana umri wa miaka 24 bado hajakamatwa ambapo alitoroka baada ya kufanya mauaji hayo na watuhumiwa sita ya familia hiyo wamekamatwa na jeshi la polisi kwa upelelezi.

KYANDO ameeleza kuwa mbinu iliyotumika, mtuhumiwa alimvizia marehemu wakati anapika chakula nje ya jiko lake na kumkata kwa kutumia panga, ambapo eneo la tukio kumekutwa na panga moja lenye damu.

Aidha KYANDO amesema upelelezi utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake, huku akitoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo hivyo na imani za kishirikiana kuwa ni imani potofu na hazina uhalisia wowote.