Kahama FM

RC Shinyanga azuia tani 400 za dengu kusafirishwa.

August 25, 2021, 12:37 pm

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dk Phillemon Sengati amezuia zaidi ya tani 400 za dengu zinazodaiwa kununuliwa kutoka kwa wakulima kwa njia ya ulanguzi zisisafirishwe nje ya mkoa huo.

Dk Sengati ameagiza shehena hiyo ambayo ilikuwa imepakiwa kwenye malori tayari kwa kusafirishwa, ishushwe na kuhifadhiwa kwenye magala ya Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) na Chama Kikuu cha Ushirika Shinyanga (Shirecu) kusubiri mnada.

Dk Sengati amesema uamuzi huo siyo tu unalinda maslahi ya wakulima watakaopata bei nzuri na yenye ushindani, bali utawezesha halmashauri na AMCOS kupata mamilioni ya fedha kupitia ushuru.

Amesema mazao yote yanayohifadhiwa katika maghala ya AMCOS na SHIRECU yataanza kuuzwa leo Jumatano Agosti 25 kwa njia ya mnada kupitia Soko la mnada kwa njia ya mtandao.