Mkoa wa Shinyanga unaendelea kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
August 18, 2021, 9:05 pm
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati amesema Serikali ya Mkoa wa Shinyanga inaendelea kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya mambo yanayoonekana katika jamii ili kuhakikisha kura za uchaguzi zinaenea katika uchaguzi Mkuu ujao.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati ameyasema hayo leo Jumatano Agosti 18,2021 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Kipindi cha Mwezi Januari hadi Juni 2021 kwenye Kikao Maalumu cha Halmashauri Kuu CCM Mkoa wa Shinyanga kilichofanyika katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu huyo wa mkoa amesema mkoa wa Shinyanga bado una maeneo mengi ya uwekezaji wa viwanda, hivyo kuwaribisha wawekezaji kuja
kuwekeza yakiwemo maeneo ya kimkakati huku akibainisha kuwa shughuli za uchimbaji madini ya Almasi katika mgodi wa Williamson Diamond Ltd ‘Mgodi wa Mwadui’ zimeanza baada ya kusimama.
Aidha amesema serikali inaendelea kufuatilia na kuwakamata wezi wa dawa za serikali, kuboresha huduma za afya zikiwemo bima ya afya, mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI na kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Katika hatua nyingine amesisitiza umuhimu wa kupanda miti ili kutunza mazingira huku akionya ukataji hovyo wa miti katika wilaya ya Kishapu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mabala Mlolwa amesema ni vyema viongozi wa CCM na wanachama wa CCM wakashirikiana na viongozi wa serikali wakiwemo wakuu wa wilaya katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi wa CCM.
Mlolwa amezitaka mamlaka zinazohusika na ukusanyaji mapato kwenda kukusanya kodi/mapato kwa njia za halali huku akionya halmashauri za wilaya zinazosababisha hati chafu kuacha uzembe kwani zinaharibu sifa ya halmashauri, mkoa na Chama Cha Mapinduzi.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu CCM Mkoa wa Shinyanga wameipokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Kipindi cha Mwezi Januari hadi Juni 2021 iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati.