Kahama FM

RC SENGATI AKUTANA NA WADAU KUPANGA MIKAKATI YA KUZUIA MAJANGA YA MOTO SHULENI….POLISI, ZIMAMOTO WATOBOA SIRI

July 16, 2021, 7:32 pm

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemoni Sengati 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemoni Sengati ameongoza kikao cha wadau kujadili mikakati ya namna ya kudhibiti majanga ya moto yanayotokea katika taasisi na shule mbalimbali.

Kikao hicho kimefanyika leo Ijumaa Julai 16,2021 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kukutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Maafisa wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Maafisa Elimu, Skauti,Waandishi wa Habari n.k ambao kwa pamoja wamekubaliana kushiriki kikamilifu katika kuzuia vyanzo vinavyosababisha kutokea kwa majanga ya moto.
Mkuu huyo wa mkoa amesema ni jukumu la kila mtu katika jamii kushiriki kuzuia vyanzo vinavyosababisha majanga ya moto kwani yanakinzana na suala la amani.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP George Kyando ameitaja mikakati inayopendekezwa na Jeshi la polisi ili kuzuia majanga ya moto katika taasisi na shule kuwa ni pamoja kila shule na taasisi iwe na walinzi makini , wale waliopitia mafunzo ya ulinzi.
Pendekezo jingine ni pamoja na shule za bweni ziwe na ulinzi shirikishi, kila shule iwe na Matron au Patroni ili kuhakikisha wanafuatilia wanafunzi wanaokuwa mabwenini na kwamba ni vizuri shule iwe na fensi/uzio, geti ili kila anayeingia pale ajulikane, ahojiwe, anaingia kufanya nini.
Kamanda Kyando pia ameshauri pia viwepo vifaa vya awali vya kuzimia moto, mfano mchanga, Fire extinguisher na pia watu wapate mafunzo ya kutumia hivyo vifaa.

Kamanda Kyando amesema pia ni lazima migogoro ya ndani na nje ya shule itatuliwe mapema sanjari na utoaji elimu ya namna ya kujikinga na majanga ya moto itolewe kwa wanafunzi.

Kwa Upande wake Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga, Inspekta Edward Lukuba amesema jeshi hilo lina wajibu wa kuzima moto na kutoa elimu ya namna ya kuzuia majanga ya moto akisema wanaendelea kutoa elimu katika shule na taasisi mbalimbali.