Waratibu Shehia acheni kutoa taarifa kwa mazoea
7 August 2023, 11:14 am
Vitendo vya udhalilishaji vinarejesha nyuma maendeleo ya wanawake na watoto
Na Vuai Juma
Waratibu wa shehia pamoja na wasaidizi wa sheria Mkoa wa kaskazini Unguja wametakiwa kuachana na tabia ya kutoa taarifa kwa mazoea hususani katika masuala ya kesi za udhalilishaji wa wanawake na watoto.
Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa bodi ya NAPAC Nd. Ali Omar Makame wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo waratibu wa shehia na wasaidizi wa sheria juu ya masuala ya udhalilishaji wa kijinsia huko mkokotoni Baraza la Mji Kaskazini “A”.
Alisema kwa kiasi kikubwa vitendo vya udhalilishaji vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku kwenye jamii zetu kutokana na waratibu hao kutoa taarifa kwa mazoea hivyo amewataka waratibu hao kuyafanyia kazi mafunzo hayo ili kufikisha ujumbe kwa jamii ili kuweza kuvikomesha vitendo hivyo.
Amefahamisha kuwa vitendo vya udhalilishaji vinarejesha nyuma maendeleo ya wanawake na watoto kutokana na athari nyingi zinazojitokeza dhidi yao hivyo ni vyema kuchukua jitihada za maksudi ili kukomesha vitendo hivyo katika shehia zao.
Nae mkufunzi wa mafunzo hayo Mw. Omar amesisitiza kuwa lengo ni kuwajengea uwezo waratibu na wasaidizi wa sheria ili wazidi kutoa taarifa za matukio ya udhalilishaji hasa kwa watoto jambo ambalo litapelekea kua na ulinzi imara dhidi ya vitendo hivyo katika jamii.
kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru jumuiya ya NAPAC kwa kuwapatia mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa vitendo katika shehia zao.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Jumuiya ya NAPAC na yamewashirikisha washiriki kutoka shehia 44 za majimbo 5 ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ambayo ni Kijini, Nungwi, Mkwajuni, Chaani na jimbo la Tumbatu.