MCHANGO WA WATAALAMU WA MAENDELEO YA JAMII TANZANIA NDANI YA MIAKA 60 YA UHURU.
December 13, 2021, 6:05 pm
Na Dr Regina Malima
Maendeleo ya jamii ni fani ya kitaalamu inayokuza demokrasia shirikishi, maendeleo endelevu na kujikita katika dhana ya uhamasishaji, ushirikishaji na kuwajengea uwezo wanajamii wote ili kuwepo na haki na usawa wa kimaendeleo kwa watu wote.
Katika utendaji, Maendeleo ya jamii ni mchakato wa kuwajengea uwezo wanajamii ili waweze kujiamini na kuwa na uwezo wa kujituma na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwa misingi ya kubaini mahitaji yao, kujua changamoto zinazowakabili, kubuni, kuandaa, kutekeleza na kusimamia mipango ya kujiletea maendeleo yao wenyewe kwa kutumia kikamilifu raslimali zilizopo katika mazingira husika na kujiletea maendeleo endelevu kwa ustawi wa maisha yao.
Dhana na falsafa ya Maendeleo ya Jamii nchini Tanzania ilianza hata kabla ya uhuru mwaka 1960 ambapo mabibi na mabwana maendeleo walibeba jukumu zima la kufanya kazi za uragibishi, uhamasishaji, tafiti mbalimbali na kuratibu na kusimamia shughuli za maendeleo ikiwemo matumizi ya chakula bora kwa familia, usafi wa mazingira, ufugaji, kilimo cha kisasa, ujasiriamali, matumizi ya teknolojia rahisi na sahihi, uvunaji wa maji ya mvua nk.
Historia inaonyesha kuwa, Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wamekuwepo na kufanya kazi nchini hata kabla ya uhuru mwaka 1960, kipindi hicho waliitwa mabibi na mabwana maendeleo na baadae kuitwa maafisa maendeleo ya jamii. Uwepo wao unaenda sambamba na wengi wao kupata mafunzo ya kitaaluma kutoka chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kilichoanzishwa mwaka 1963.
Wataalamu wa maendeleo ya jamii walipata/wanapata ujuzi na maarifa ya kitaaluma kutoka katika vyuo mbalimbali na hivyo kufanya kazi na kuifikia jamii ili kutatua changamoto zao na kupata masuluhisho ya kudumu kwa kuhamasisha na kuelimisha jamii kuondokana na mila, fikra potofu na desturi zinazoleta madhara kama vile unyanyasaji wa kijinsia, mauaji ya albino na ukeketaji wa wanawake, ndoa na mimba za utotoni.
Wataalamu wa maendeleo ya jamii nchini kwa sasa wanafanya kazi katika Halmashauri zetu katika ngazi za Mikoa, Wilaya, kata na hata vijiji na katika asasi mbalimbali za kiraia katika kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo.
Dhamira kuu na msingi wa watendaji wa maendeleo ya jamii ni kuongeza ushiriki wa watu katika jamii kama msingi na chachu ya juhudi zozote za maendeleo na kuwahamasisha kuwa sehemu ya maendeleo kwa kuzingatia umakini wa watu na uwezeshaji wa jamii ambayo iko katika mazingira magumu, inayokandamizwa, na kuishi katika umaskini ili jamii za namna hiyo ziweze kupiga hatua na kuondokana na umaskini katika maeneo yao.
Miongoni mwa majukumu yao ni pamoja na; Uhamasishaji mpana wa watu kushiriki katika maendeleo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ya ndani na kitaifa, Kuwezesha jamii na wadau wa maendeleo kufanya kazi pamoja katika kufikia malengo ya maendeleo ya jamii kwa misingi endelevu, Kusimamia utekelezaji wa miradi/programu za maendeleo ya jamii zinazofadhiliwa na serikali na wadau wengine wa maendeleo, Kueneza na uimarishaji wa asasi za msingi za jamii, Vyama vya Akiba na Mikopo vya Vijiji (VSLA), SACCOS, VICOBA na aina nyingine za vikundi vinavyozingatia jamii, aidha Maafisa Maendeleo ya Jamii katika mamlaka za serikali za mitaa wanasajili na kusimamia shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOS) na kuratibu na kusimamia shughuli chini ya baraza la taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi katika mamlaka za serikali za mitaa na kushauri mamlaka za serikali za mitaa juu ya utekelezaji wa sheria zinazohusiana na afua mbalimbali za maendeleo ya jamii.
Kuna mafanikio makubwa nchini kutokana na mchango wa taaluma ya maendeleo ya jamii kwa ujumla kabla na baada ya uhuru kwa wataalamu hawa kutoa mchango mkubwa katika kutekeleza majukumu yao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo nchini katika kuwaletea wananchi maendeleo katika maeneo ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, usawa wa kijinsia, upatikanaji wa haki za wazee na watoto na uratibu wa Mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yamekuwa yakishughulika na masuala ya maendeleo ya jamii nchini.
Sekta ya Maendeleo ya Jamii imewezesha wananchi kupokea, kushiriki katika kupokea shughuli za kimaendeleo toka awali ikiwemo kushughulikia uhamasishaji wa malezi bora katika familia, ujenzi wa nyumba bora na vyoo, kupeleka watoto shule, ujenzi wa vituo vya afya na namna ya kutumia huduma za afya, ujenzi wa nyumba bora za kuishi na vyoo.
Aidha, na katika miaka ya hivi karibuni sekta ya maendeleo ya jamii kwa kutumia wataalam wake wameendelea kutoa hamasa katika jamii katika ujenzi wa Shule za Sekondari, upatikanaji wa madawati, kuchangia na kumiliki program za Maendeleo mbali mbali ikiwemo miradi iliyoanzishwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Ndani ya miaka 60 ya uhuru, Chama cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA) kimeanzishwa nchini Tanzania mwaka 2017 na kusajiliwa ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Sheria ya Vyama (Cap, 337 RE 2002) kwa Cheti cha Usajili Nambari SA 21457 kikiwa ni chama cha kitaaluma cha kujitolea, kisicho cha kiserikali, kisichoegemea upande wowote chenye dhamira ya kukuza na kulinda Taaluma ya Maendeleo ya Jamii kwa maendeleo endelevu ya watu nchini Tanzania.
Aidha, chama hiki kinalenga kukuza na kuboresha masilahi ya kitaaluma ili kuwawezesha wataalamu wa maendeleo ya jamii nchini kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa na kutekeleza majukumu yao kwa kanuni za kitaaluma bila ya fani yao kuingiliwa na wataalamu wa fani zingine.
Katika kulisimamia hili, CODEPATA inaandaa kanuni za miiko na maadili ya kitaaluma zitakazosimamia taaluma ya maendeleo ya jamii nchini ili kulinda taaluma hii yenye mchango mkubwa katika nchi hivyo kuendelea kutoa matokea chanya katika jamii.
Kwa sasa Chama hiki kina wanachama zaidi ya mia nne (400) nchini huku asilimia zaidi ya 90% ya wanachama wake wakiwa ni waajiriwa katika sekta ya umma katika halmashauri mbalimbali nchini na wengine wakifanya kazi katika taasisi zisizo za kiserikali na hivyo wataalamu hawa kuwa na nafasi ya pekee ya kufanya kazi kwa karibu pamoja na jamii.
Chama kina uhusiano wa karibu na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kama Mlezi wake katika kuhakikisha taaluma ya maendeleo ya jamii inasimama katika misingi yake kwa kutoa huduma bora kwa jamii.
Taaluma ya Maendeleo ya Jamii ni mhimili mkuu katika maendeleo ya nchi na hivyo kuwa nyenzo ya kutatua changamoto mbalimbali kuharakisha maendeleo ya nchi katika jamii kwa kujenga uchumi endelevu kwa maendeleo ya watu.
Ili maendeleo yawe na tija, ni vizuri wataalamu wa maendeleo ya jamii kuendelea kumuunga mkono Rais wa awamu ya sita Mh Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kazi kwa ubunifu kwa kuzingatia misingi iliyomo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 hadi 2025/26, Sera ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996, mikakati mbalimbali ya kisekta, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020/2025 pamoja na kutumia matokeo ya tafiti zinazofanywa na vyuo na taasisi mbalimbali nchini.
Kwa kuzingatia mipango na mikakati hii ya kitaifa, Wataalam wa maendeleo ya jamii wanategemewa kuwa sehemu ya kuhamasisha na kushirikisha jamii katika utekelezaji wake kikamilifu na hivyo kuleta maisha bora kwa wananchi; amani, ajira kwa vijana, utulivu na umoja; jamii iliyoelimika na inayopenda kujifunza; na uchumi imara na shindani.
Aidha, wananchi wanapaswa kushiriki katika mchakato wa maendeleo yao wenyewe kuweza kubuni miradi inayokidhi mahitaji yao halisi na hivyo kuwa na mchakato wa maedeleo endelevu.
Hii pia ndiyo njia halisi ya uhuru wa kweli kwani wanachi hushiriki katika kuamua juu ya maedeleo yao bila kulazimishwa. Dhana na falsafa hii ni sambamba na itikadi ya serikali ya kupeleka madaraka kwa wanachi kwa ugatuzi kupitia serikali za mitaa.
Mchakato wa maendeleo katika ngazi ya jamii ni mbali na sera, sheria na miongozo mabalimbali ni lazima usaidiwe na kuongozwa na kuratibiwa na wanataaluma ambaye ana mawanda mapana katika kuifahamu jamii na kuwa tayari si tu kuchangamana na jamii bali pia kushirikiana na taaluma nyingine kimkakati na kimahususi katika kutambua changamoto, vikwazo, fursa na kuchagiza maendeleo kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa.
Mwandishi wa Makala hii ni:
Dr Regina Malima
Tel:0758-515613
E-mail:regina.malima@yahoo.co.uk