MEDIA DAY
Kahama FM

SERIKALI yapigilia msumari waandishi kuwa na Diploma.

May 3, 2021, 10:43 pm

Na Kijukuu Cha Bibi K-Arusha.

SERIKALI imesisitiza kuwa kufikia mwezi wa kumi na mbili mwaka huu sheria iliyopitishwa ya kuwataka waandishi wa Habari wawe na kiwando cha elimu ngazi ya stashahada itaanza kutumika na kwamba waandishi ambao hawana elimu ngazi ya Stashahada watumie miezi hii iliyobaki kujiunga na vyuo vya uandishi wa Habari.

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na michezo Innocent Bashungwa akitoa hotuba siku ya uhuru wa vyombo vya habari jijini Arusha.

Wito huo umetolewa leo jijini Arusha na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na michezo Innocent Bashungwa katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya Habari duniani yaliyofanyika kitaifa katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano Jijini Arusha (AICC)

Bashungwa amesema kuwa Serikali ina dhamira kubwa ya kuuinua Tasnia ya Habari nchini na kwamba swal la kuwataka waandishi kusoma na kuwa na ngazi ya shahada waliipa muda wa miaka mtano na kwamba mwaka huu 2021 ndiyo mwisho wa muda uliokuwa umewekwa.

Sauti ya Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na michezo Innocent Bashungwa akiongelea swala la waandishi kujiendeleza kielimu.
Baadhi ya waandiishi wa habari za Mitandaoni (Alternative Media) wakifuatilia hotuba ya waziri wa habari (Hayupo pichani)

Sambamba na hayo Bashungwa amewahakikishia waandishi wa Habari kuwa Serikali ya awamu ya Sita itawapa ushirikiano kuhakikisha waandishi wanafanya kazi zao bila kikwazo kwani anatambua wapo baadhi ya  maafisa Habari wa serikali wamekuwa wagumu kutoa taarifa kwa waandishi wa Habari hata kama wakionyeshwa vitambulisho vilivyotolewa na serikali.

Sauti ya Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na michezo Innocent Bashungwa akiongelea swala la changamoto kwa waandishi

Awali akitoa taarifa ya ujumla ya mwenendo wa uhuru wa vyombo vya Habari nchini  Kaimu mwenyekiti wa jukwaa la wahariri Tanzania Deodatus Balile amesema kuwa mwelekeo wa uhuru wa vyombo vya Habari umekuwa siyo wa kuridhisha kwani ndani ya miaka mitano mfululizo Tanzania imekuwa na anguko la uhuru wa vyombo vya Habari.

Sauti ya Kaimu mwenyekiti wa jukwaa la wahariri Tanzania Deodatus Balile

Akielezea mambo yaliyosababisha  kushuka kwa mwenendo wa uhuru wa vyombo vya Habari nchini Balile amesema kuwa ni Pamoja na kuvifungia vyombo vya Habari na kuvitoza faini kiholela  na kupigwa kwa waandishi wa Habari huku akitolea mfano wa mwandishi wa Gazeti la mwananchi aliyepigwa na askari wa JKU Visiwani Zanzibar.

Kaimu mwenyekiti wa jukwaa la wahariri Tanzania Deodatus Balile akielezea sababu ya anguko la uhuru wa vyombo vya habari Nchini.

Nao baadhi ya waandishi wa Habari waliohudhuria maadhimisho hayo Albert Sengo kutoka jijini Mwanza na Asha Banni kutoka Mkoani Mara wameiomba serikali kusimamia sheria zinazowalinda waandishi wa Habari na jamii itambue mchango wa wanahabari katika kuleta maendeleo ya nchi.

Baadhi ya wadau waliohudhuria maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari yaliyofanyika jijini Arusha katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Arusha (AICC)

Siku ya uhuru wa vyombo vya Habari Duniani huazimishwa kila Tarehe 3 ya mwezi wa 5 ya kila mwaka huku kaulimbiu ya mwaka huu ikisema ”Habari kwa Faida ya Umma” ambapo nchini Tanzania imefanyika kitaifa jijini Arusha.