Bunda FM Radio
Bunda FM Radio
25 November 2026, 11:31 am

“SERIKALI itaendelea kubeba gharama za msingi kwa ajili ya chanjo na utambuzi wa mifugo kama hatua ya kumlinda mfugaji mdogo dhidi ya gharama za utunzaji na hatari za magonjwa ya mifugo.” Katibu Tawala Ndugu Shabani Manyama
Na Jesca mwita
Serikali ya Halmashauri ya mji wa Bunda amezindua rasmi zoezi la utoaji wa chanjo ya Homa ya mapafu kwa Ng’ombe na Sotoka kwa mbuzi na kondoo. Chanjo hii ilianza kutolewa tarehe 09 Novemba 2026 na itahitimishwa tarehe 12 Desemba 2026.
Uzinduzi huo umefanywa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda Ndugu Shabani Manyama kwa niaba ya Mh Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dkt. Khalfany Haule. Amesema kuwa wafugaji wanatakiwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vilivyotengwa kwa mujibu wa ratiba ya wataalamu ili mifugo ipate chanjo kwa wakati, na kulinda afya na kuzuia magonjwa yanayodhoofisha mifugo na kupunguza uzalishaji wa maziwa, nyama na kipato cha mfugaji

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Bunda Ndg. Said Ramadhani aliwashukuru wafugaji waliojitokeza kwa wingi kuchanja mifugo yao na kuwataka kupeleka salamu kwa wafugaji wengine ambao hawakufika ili nao waweze kupeleka mifugo yao kuchanja.

Naye Kaimu mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Mji wa Bunda Ndg. Siana amesema kuwa inatarajia kuchanja Ng’ombe 69,372, kondoo 35,859 na mbuzi 30,670 ambapo hadi sasa Ng’ombe waliochanjwa ni 4,775 mbuzi na kondoo 5,112.
