Vwawa FM Radio
Vwawa FM Radio
September 21, 2025, 8:40 am

Ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali la matumizi ya nishati safi
Na Stephano Simbeye
KIKOSI cha Jeshi la kujenga Taifa (JKT) 845KJ Itaka wilaya ya Mbozi mkoani Songwe kimeanza kufundisha jinsi ya kutengeneza mkaa mbadala kwa kutumia taka za shambani.
Mkuu wa Kikosi hicho, Kanali Gervas Chitola amesema mafunzo hayo yatakuwa yanatolewa kwa askari wapya wanaoingia kwa mujibu wa sheria,
Amesema hayo kwenye hafla kuhitimu kuwaaga waliomaliza mafunzo ya mujibu wa sharia jana ambapo mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe Jabiri Makame alikuwa mgeni rasmi.
Aidha kanali Chitola amesema mafunzo hayo yanatolewa kutekeleza agizo la serikali la kutaka taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 kutumia Nishati mbadala ili kuhifadhi mazingira.
Aidha Kanali Chitola amebainisha kwamba tayari kikosi hicho kimepata mashine za kisasa zitakazotumika kuandaa mkaa huo unaoweza kutumika pia majumbani.
Naye Mkurugenzi wa mawasiliano wa JKT, Kanali Juma Issa Mlai amesema mafunzo ya awali ya kijeshi kwa mujibu wa sheria yana lengo la kuwandaa vijana, kuwa na moyo wa uzalendo, umuhimu wa kutumia muda vizuri, ukakamavu na ujasiri.
Kwa upande wao wahitimu hao wamesema mafunzo waliyoyapata yamewasaidia kufahamu stadi za maisha na yamekuwa chachu na msaada katika maisha Yao, ikiwemo kuwajengea mahusiano na wengine na kuishi kwa upendo.
Akihutubia kabla ya kufunga mafunzo hayo Mkuu wa Mkoa Songwe Jabiri Omari Makame amewasihi wahitimu hao kuepuka kujiingiza kwenywe makundi mabaya ya matumizi ya mitandao bali waitumie mitandao kama fursa.