Savvy FM
Savvy FM
17/03/2026, 13:30

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, ndugu Seleman Msumi, amesema malezi bora ni kielelezo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu katika jamii.
Na Mariam Mallya
Msumi ameeleza hayo jijini Arusha kwenye kongamano lililowakutanisha makundi ya malezi na walezi kutoka halmashauri nne za mkoa wa Arusha, ambapo amesema serikali kwa kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali kupitia mwongozo wa malezi itasaidia kupunguza matukio ya ukatili katika jamii.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, bwana Victor Rugarabamu, amelipongeza shirika la SOS Children’s Village kwa kuanzisha vikundi hivyo vya malezi katika mkoa wa Arusha, akisema vikundi hivyo vitasaidia kuimarisha malezi bora katika jamii.
Awali akizungumza, Meneja wa SOS Children’s Village mkoa wa Arusha, bwana Mpeli Kalonge, amesema lengo kubwa ni kutoa malezi mbadala na kuimarisha ulinzi wa mtoto pamoja na kupinga matukio ya ukatili katika jamii.
Naye Veronika Kidemi, mmoja wa waathirika wa vitendo vya ukatili, ameitaka jamii kupaza sauti na kushirikiana kupambana na matukio ya ukatili yanayotokea katika jamii.