Savvy FM

Ushiriki wa baba katika malezi watajwa kuwa changamoto

16/03/2026, 14:57

Mtaalam wa masuala ya ulinzi wa mtoto Husna Selungwi akizungumza na waandishi wa habari. Picha na Mariam Mallya

Wadau wa masuala ya malezi na makuzi ya watoto wamesema ushiriki mdogo wa wanaume katika malezi ya watoto bado ni changamoto kubwa katika jamii, hali inayoweza kuathiri ukuaji na ustawi wa watoto.

Na Mariam Mallya

Mtaalam wa masuala ya ulinzi wa mtoto Husna Selungwi kutoka shirika la SOS Children’s Villages Tanzania amesema ushiriki wa baba katika malezi ni muhimu kwa sababu unasaidia kujenga uhusiano wa karibu kati ya mtoto na wazazi wake, hali inayochangia ustawi wa mtoto kimwili, kiakili na kihisia.

Bi Husna ameyasema hayo wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu masuala ya malezi na makuzi ya mtoto yaliyofanyika jijini Arusha ambapo amesema watoto wengi hutamani kuwa karibu na baba zao, na baba pia hutamani kuwa karibu na watoto wao. Hivyo ushiriki kikamilifu katika malezi husaidia kuimarisha mahusiano ya familia.

Sauti ya Mtaalamu wa masuala ya ulinzi wa mtoto Husna Selungwi.

Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo wamesema pamoja na jitihada za serikali kutekeleza mpango wa maendeleo ya awali ya mtoto, bado wanaume wengi hawashiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wao.

Sauti za baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo

Aidha, imeelezwa kuwa kupitia programu mbalimbali za malezi imebainika bado kuna uelewa mdogo kwa baadhi ya wanaume kuhusu wajibu wao katika malezi ya watoto.
Hivyo kutokana na hali hiyo, waandishi wa habari wamehimizwa kutumia majukwaa yao kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa wanaume kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama na yenye upendo.