Radio Kwizera

Asante Africa Foundation yasaidia wanafunzi 101 Geita

April 13, 2026, 6:54 pm

Baadhi ya Wawakilishi wa Kampuni na Taasisi zilizotoa vifaa kwa wanafunzi 101, Geita. Picha na Clement Shawishi

Wanafunzi 101 kutoka shule za sekondari Dhahabu, Evarist na Lwamugasa wamepatiwa vifaa mbalimbali vya kujiendeleza kitaaluma dhamira kuu ikiwa ni kuongeza ufanisi wa sera ya elimu bure.

Na Clement Shawishi- Geita

Afisa Elimu kata ya Nyarugusu wilayani Geita Bw. Robert Roth amewasihi wazazi na Bodi za shule kuongeza nguvu ya ufuatiliaji na utatuzi wa vikwazo kwa wanafunzi shuleni ili kufikia lengo la kuinua sekta ya elimu.

Bw. Roth amesema hayo wakati akipokea ufadhili wa vifaa vya masomo kwa wanafunzi 101 wa kidato cha kwanza katika shule 3 za sekondari uliotolewa na Asante Africa Foundation kwa ushirikiano na mgodi wa Mwamba Mining.

Amewaomba wazazi na walezi kuwajibika kwa nafasi yao kwa kufuatilia mienendo ya watoto kabla, wakati na baada ya masomo ili kuhakikisha msaada wanaopewa unachochea maendeleo ya watoto kitaaluma.

Meneja wa Asante Africa Foundation Bw. Florence Thomas amebainisha kuwa wanafunzi waliofikiwa ni kutoka shule ya sekondari Dhahabu, Evarist na Lwamugasa dhamira kuu ikiwa ni kuongeza ufanisi wa sera ya elimu bure.

Baadhi ya wanafunzi wakikabidhiwa vifaa watakavyotumia kwenye masomo yao. Picha na Clement Shawishi

Meneja wa Mgodi wa Mwamba Mining Bw. Calvin Habil amesema kampuni hiyo inashiriki katika mradi huo kutekeleza sera yake isemayo madini yaliyopo chini ya ardhi yawanufaishe watu waliopo juu ya ardhi.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Nyarugusu Bw. Lusekelo Mwaikenda amepongeza wadau kwa ufadhili huo na kusisitiza kuwa ofisi yake imeweka mipango thabiti kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekatisha masomo.

Ufadhili huo unahusisha msaada wa sare za shule, madaftari, mabegi pamoja na vifaa vya usafi na baiskeli kwaajiri ya usafiri kwa wanafunzi wanaotoka mbali hususani wa kidato cha kwanza kutoka familia zenye kipato cha chini.