sensa
Kahama FM

IRINGA:NBS yatoa mafunzo ya Sensa ya watu na makazi kwa wahariri wa redio za kijamii.

June 16, 2022, 1:38 pm

 

IRINGA

Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha na kutoa elimu ya sensa ya watu na makazi ili kuhakikisha zoezi linafanikiwa kuanzia ngazi ya vijiji,kata,wilaya mkoa hadi taifa.

Wito huo umetolewa leo mkaoni Iringa na Mtaalamu wa idadi ya watu kutoka Ofisi ya taifa ya Takwimu Hellen Siriwa wakati akiongea na wahariri wa redio za kijamii nchini katika mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Ofisi ya taifa ya takwimu kwa kushirikina na mtandao wa redio za kijamii nchini (TADIO).

Siriwa Amesema kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kutoa elimu kwa wananchi kwakuwa redio hizo hususan za kijamii zinawafikia kwa urahisi wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Ameongeza kuwa wananchi wanaviamini sana vyombo vya habari na kwamba redio za kijamii zikiweka nguvu katika elimu ya sensa ya watu na makazi zoezi litafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa mwaka huu.

Sambamba na hayo Siriwa ameongeza kuwa sensa itasaidia kupanga shughuli za maendeleo kitaifa zikiwemo upatikanaji wa maji,Miundo mbinu,Elimu na afya katika ngazi zote.

Kwa upande wao baadhi ya wahariri kutoka redio za kijamii nchini wameishukuru Ofisi ya taifa ya Takwimu na mtandao wa redio za kijamii (TADIO) kwa mafunzo hayo na wamehaidi kutoa elimu kwa kina kuhusu sensa ya watu na makazi kupitia redio zao.

Mafunzo hayo yanayoendelea mkoani Iringa Katika chuo kikuu kishiriki cha elimu Mkwawa  yameshirikisha redio za kijamii hamsini (50) zilizo katika mtandao wa redio za kijamii (TADIO) na ambazo zipo katika maudhui ya redio za Kijamii.