Vwawa FM Radio

Madereva kudumisha amani, wamkaribishaRC mpya Songwe

August 11, 2025, 8:00 pm

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mh. Jabiri Omari Makame (kushoto), akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mh. Hamad Mbega (kulia), pamoja na wananchi wakishiriki mbio za taratibu (jogging) zilizoandaliwa na kikundi cha waendesha bodaboda, bajaji na maguta Mkoa wa Songwe. Picha Stephano Simbeye

Waendesha usafiri Songwe wamemkaribisha RC mpya wa Songwe na kuahidi kulinda amani Mkoani humo, huku wakisisitiza kushirikiana na serikali na kutojihusisha na makundi ya kihalifu.

Na Stephano Simbeye

Waendesha bodaboda, maguta na bajaji wamesema hawako tayari kujiunga na makundi maovu ya kihalifu, badala yake wameahidi kushirikiana na serikali katika kudumisha amani na usalama wa nchi.

Kauli hiyo imetolewa Agosti 9 mwaka huu kupitia risala iliyosomwa na Katibu wa Bajaji, Abel Mwambene, katika hafla ya mbio za taratibu iliyoandaliwa na makundi hayo kwa lengo la kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mh.Jabiri Omari Makame.

Sauti ya Katibu wa Bajaji Wilaya ya Mbozi Abel Mwambene

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bajaji Wilaya ya Mbozi, Charles Mutare, amesema hatua ya serikali kutambua kazi ya waendesha bajaji, bodaboda na maguta kama kazi halali imewapa nguvu na ari zaidi ya kuendelea kufanya shughuli zao kwa bidii.

Sauti ya Mwenyekiti wa Bajaji Wilaya ya Mbozi, Charles Mutare

Naye Mwenyekiti wa Bodaboda Mkoa wa Songwe, Omary Mbuba, amesema kupitia kazi ya uendeshaji bodaboda wamefanikiwa kuchangia maendeleo, ikiwemo kujenga nyumba za kuishi na kusomesha watoto wao.

Sauti ya Mwenyekiti wa Bodaboda Mkoa wa Songwe, Omary Mbuba

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Jabiri Omari Makame, amezitaka taasisi zinazoshughulikia masuala ya usafirishaji hususan LATRA, kutozubugudhi waendesha bodaboda, bajaji na maguta kwa kuwakamata au kuwanyang’anya funguo. Badala yake, ameshauri watumie viongozi wao kuwasisitiza kulipa tozo na ada za serikali kwa wakati.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Jabiri Omari Makame
Mkuu wa Mkoa wa Songwe akipokea zawadi ya Mbuzi kutoka kikundi waendesha bodaboda, bajaji na maguta Mkoa wa Songwe