Vwawa FM Radio
Vwawa FM Radio
August 9, 2025, 9:12 pm

viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na wadau wengine wa uchaguzi wamekutana Mbozi kuweka mikakati ya kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na haki, huku DC Hamad Mbega akitoa onyo kali kwa wavunjifu wa amani
Na Stephano Simbeye
Serikali wilayani Mbozi, mkoa wa Songwe, imesema haitamvumilia mtu yeyote atakayejaribu kuvuruga amani katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Kauli hiyo imetolewa Agosti 8 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Hamad Mbega, wakati akitoa salamu za serikali katika kikao cha kupitia ratiba ya Uchaguzi Mkuu iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Kikao hicho kimehusisha viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na wadau wengine wa uchaguzi.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Karl uliopo mjini Vwawa. Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mbega amesema:
Aidha, Mbega amesema uchaguzi ni takwa la kikatiba na ni lazima ufanyike ili kupata viongozi watakaoongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo baada ya muda wa uongozi kumalizika. Alisisitiza hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kuzuia mchakato huo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wilaya ya Mbozi, Enock Mwalukasa, amesema matatizo mengi ya uchaguzi huanzia kwa mawakala hivyo alipendekeza mawakala waapishwe katika maeneo yao ya kata.

Akizungumzia suala la uchukuaji na urejeshaji wa fomu, Mwalukasa ameonya dhidi ya mchezo wa kufunga ofisi za watendaji uliowahi kutokea katika chaguzi zilizopita, akisisitiza kwamba jambo hilo lisijirudie mwaka huu.

Viongozi wa madhehebu ya dini wamesema wanatarajia uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa haki, amani na utulivu, huku wakiongeza kuwa wamekuwa wakiombea hali hiyo idumu.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo ya Vwawa na Mbozi, Danny Tweve, amesema tume imejipanga kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki akiongeza kuwa hakutakuwa na visa vya kufunga ofisi za umma kwa visingizio vyovyote, na kuwataka wadau kutoa taarifa mapema iwapo wataona viashiria vya hali hiyo.