Vwawa FM Radio

Siwale aweka historia ya kugombea Urais kutoka Songwe

July 17, 2025, 2:03 pm

Picha ya Nkunyuntila Siwale. Picha na Kennedy Sichone

Mzee Siwale (80) kutoka Mbozi, Songwe, achukua fomu ya urais kupitia CUF, akiweka historia ya kuwa mgombea wa kwanza kutoka mkoa huo.

Na Stephano Simbeye

Mwanachama wa Chama cha Wananchi CUF kutoka wilaya ya Mbozi, mkoa wa Songwe, Nkunyuntila Siwale mwenye umri wa miaka 80 ameandika historia kwa kuwa mgombea wa kwanza kutoka mkoa huo kuchukua fomu ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.

Siwale amechukua na kurejesha fomu ya kugombea urais Julai 15, 2025 mbele ya viongozi wa CUF wa mkoa wa Songwe, katika hafla iliyofanyika Mlowo wilayani Mbozi mkoa wa Songwe.

Amesema hatua hiyo imelenga kutoa nafasi kwa vijana kupata ajira, kupata viongozi makini pamoja na kusimamia misingi ya haki na usawa kwa watanzania wote.

Sauti ya Nkunyuntila Siwale

Mwenyekiti wa CUF Mkoa wa Songwe, Enock Mwalukasa amesema kuwa hatua ya Siwale ni ya kihistoria na imeongeza thamani ya mkoa huo katika siasa kwani amekuwa wa kwanza kutoka mkoa wa Songwe kuchukua fomu ya kuwania urais.

Sauti ya Mwenyekiti wa CUF Mkoa wa Songwe, Enock Mwalukasa

Naye Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa wa CUF ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF Mkoa wa Mbeya, Yassin Mlotwa, amesema chama hicho kimeamua kushiriki kikamilifu uchaguzi mkuu ujao ili kuhakikisha wananchi wanapata viongozi wanaojali maslahi yao.

Sauti ya Yassin Mlotwa akieleza sababu za Chama cha CUF kushiriki uchaguzi mkuu.

Mlotwa amesema kuwa zoezi la kuchukua fomu kwa nafasi ya urais kupitia CUF limehitimishwa rasmi Julai 15, 2025 majira ya saa 10 jioni ambapo jumla ya wagombea sita wamejitokeza kuchukua fomu ya urais kupitia chama hicho. Ametaja majina ya wagombea wote waliowasilisha fomu zao.

Sauti ya Yassin Mlotwa akitaja majina ya wagombea.

Aidha, Mlotwa ameongeza kuwa zoezi la uchukuaji wa fomu kwa nafasi ya ubunge na udiwani linaendelea na amewahimiza wanachama wengine kuchangamkia fursa hiyo ya uongozi.