Vwawa FM Radio
Vwawa FM Radio
June 11, 2025, 6:38 pm

Watoa huduma za afya Wilaya ya Mbozi wamepatiwa mafunzo ya lugha ya alama ili kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu wa kusikia na kuhamasisha ushiriki wao katika jamii
Na Stephano Simbeye.
Watoa huduma za afya kutoka kata tano za Wilaya ya Mbozi wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya lugha ya alama, na wameahidi kushirikisha wenzao waliobaki vituoni ili kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu wa kusikia.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamefanyika katika ukumbi wa Simple Palace mjini Vwawa, yakiandaliwa na shirika la ADP Mbozi kwa kushirikiana na DSW kupitia mradi wa SAfA. Washiriki wametoka katika vituo vya afya vya kata za Itaka, Nambinzo, Igamba, Idiwili na Hezya.
Kupitia mafunzo hayo, watoa huduma wameongeza uelewa juu ya mawasiliano jumuishi, na sasa wanajipanga kutumia elimu hiyo kuboresha huduma kwa makundi maalum katika jamii.
Mmoja wa wahudumu hao kutoka zahanati ya Idiwili Catherini Luhumulu amesema atayapeleka mafunzo hayo kwa wenzake anaofanya nao kazi ili nao waweze kufahamu namna ya kuwahudumia watu wa aina hii.
Naye Lugendo Abel toka kituo cha Afya Hezya amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuondoa changamoto ya kushindwa kuwasiliana na walemavu wanaotumia lugha ya alama.