Vwawa FM Radio
Vwawa FM Radio
June 5, 2025, 1:57 pm

Wadai kukerwa na harufu mbaya, mwenyekiti wa madereva atoa ya moyoni
Na Anyisile Fredy
Baadhi ya abiria wa bodaboda na bajaji mjini Vwawa Mbozi mkoani Songwe wameendelea kuzungumzia kero wanazopata kwa madereva wachafu wa vyombo hivyo.
Akizungumzia suala hilo, abiria Daniel Ngajilo kutoka Ichenjezya amesema baadhi ya madereva wanavaa makoti machafu yanayonuka kwa siku nyingi bila kufuliwa.
Naye dereva mstaafu wa bodaboda wilayani Mbozi, Jack Mponda amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na ameshauri kutolewa kwa elimu ya usafi mara kwa mara wanapokutana vijiweni.
Amesema abiria wengine wanatamani washuke kwenye pikipiki ama bajaji kutokana na harufu mbaya ya dereva jambo ambalo halipendezi kwa madereva wa bodaboda ama bajaji.
Akizungumzia changamoto hiyo, Mwenyekiti wa madereva wa bodaboda wa kijiwe namba 10 Vwawa, Saidi Lwenje amekiri kuwapo kwa baadhi ya madereva wasiozingatia usafi.
Aidha amewataka madereva kuzingatia usafi wa mwili na mavazi kila siku ikiwa ni pamoja na kuoga asubuhi na kuvaa nguo safi.